Delap asikilizia dili Fulham, mshkaji wake akitua
Muktasari:
- Delap amekuwa akipitia wakati mgumu tangu alipotua Chelsea dirisha lililopita la usajili kutokana na kutokuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza jambo ambalo limekuwa likiuweka mustakabali wake shakani.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England na Chelsea, Liam Delap, mwenye umri wa miaka 23, anaweza kujiunga na Fulham katika dirisha hili la usajili iwapo tu kocha wake wa zamani aliyemnoa walipokuwa Ipswich Town, Kieran McKenna, atachukua nafasi ya Marco Silva.
Delap amekuwa akipitia wakati mgumu tangu alipotua Chelsea dirisha lililopita la usajili kutokana na kutokuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza jambo ambalo limekuwa likiuweka mustakabali wake shakani.
Kinachoelezwa ni kwamba mchezaji huyo tayari ameshafikia uamuzi wa kuondoka katika kikosi hicho ambacho msimu ujao hakitakuwa miongoni mwa timu zinazocheza mashindano ya klabu Ulaya, na huenda akatimkia timu nyingine hata kama itakuwa haichezi michuano hiyo. Kabla ya kutua Chelsea Delap alikuwa staa anayeongoza mashambulizi kikosini Ipswich Town. Mkataba wake Chelsea unamalizika Juni 2031.
Julian Alvarez
JITIHADA za Barcelona kumsajili mshambuliaji wa kimtaifa wa Argentina, Julian Alvarez, 26, kutoka Atletico Madrid zinadaiwa kukwama na kwa sasa timu yake inapanga msimu ujao kuwa na mchezaji huyo katika kikosi chake. Ingawa Arsenal pia wanamhitaji, Alvarez hafikirii kuhamia London, ambapo akili yake ameiwekeza Barcelona kwenda kuchukua mikoba ya Robert Lewandoski aliyeondoka baada ya mkataba kumalizika. Mkataba wake unamalizika 2030.
Rafael Leao
WINGA wa Ureno na AC Milan, Rafael Leao, mwenye umri wa miaka 26 anadaiwa kuwaambia mabosi wake kwamba anataka changamoto mpya msimu ujao. Mchezaji huyo anaamini kwamba kuhamia Ligi Kuu England au Hispania (La Liga) litakuwa jambo jema kwake. Leao amekuwa katika kikosi cha kwanza cha Milan tangu alipotua 2019 na ameendelea kumiliki namba yake. Mkataba unaisha Juni 2028.
Yan Diomande
RB Leipzig ina imani kuwa winga wa kimataifa wa Ivory Coast, mwenye umri wa miaka 19, Yan Diomande, atasalia klabuni hapo msimu ujao licha ya Liverpool kuongeza juhudi za kumsajili. Diomande anaendelea kuzitoa udenda timu mbalimbali Ulaya tangu alipojiunga na kikosi hicho majira ya joto mwaka jana. Mchezaji huyo anamaliza mkataba wake Juni 2030.
Ewen Jaouen
NEWCASTLE United inatarajiwa kufanya usajili wa kwanza wa majira ya joto baada ya kudaiwa kukubaliana ada ya Pauni 24 milioni kwa ajili ya kumnyakua kipa wa Mfaransa mwenye miaka 20, Ewen Jaouen kutoka Stade de Reims. Mchezaji huyo anatarajiwa kuondoka katika kikosi hicho baada ya kupokea ofa nyingi tangu msimu uliopita kutokana na mafanikio aliyoonyesha uwanjani.
Luis Fernando
HULL City waliopanda Ligi Kuu England hivi karibuni wanaangalia uwezekano wa kumsajili winga wa kimataifa wa Venezuela, Luis Fernando Carrero kutoka Deportivo Tachira kabla ya kumtoa kwa mkopo kwenda NK Maribor. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 ameziweka mkao wa kula timu nyingi za England kutokana na kiwango chake bora huku umri wake ukiongeza ushawishi sokoni. Mkataba anamaliza 2028.
Hayden Hackney
KIUNGO wa kimataifa wa England na Middlesbrough, Hayden Hackney mwenye umri wa miaka 23 ameiweka Everton mkao wa kula na tayari imewasiliana na Middlesbrough kwa ajili ya kumsajili dirisha hili, ingawa ofa inayodaiwa kutoa bado iko mbali na thamani yake. Hackney pia anazivutia timu mbalimbali za Ufaransa ambazo zinadaiwa kugonga hodi klabuni kwake kuulizia uwezekano wa kumnasa.
Luka Vuskovic
KOCHA wa Tottenham Hotspur, Roberto De Zerbi, anataka beki wa kimataifa wa Croatia, Luka Vuskovic mwenye umri wa miaka 19 aondoke klabuni msimu huu wa joto. Uamuzi huo wa De Zerbi unalenga kumfanya nyota huyo chipukizi kwenda kuendelea kupata uzoefu kwa mkopo katika klabu nyingine au kumuuza jumla. Msimu uliopita Vuskovic aliichezea Hamburger SV ya Ujerumani kwa mkopo. Mkataba wake na Spurs unamalizika Juni 30, 2030.