De Bruyne aachwa aamue hatima yake Manchester City
Muktasari:
- Kiungo huyo wa Kibelgiji amebakiza miezi mitano kwenye mkataba wake na tayari amekuwa akihusishwa na klabu kibao za Saudi Arabia na Marekani zinazohitaji saini yake. De Bruyne amecheza mechi 23 msimu huu na aliwahi kufichua kwamba yupo tayari kuendelea kubaki Etihad.
MANCHESTER City imeripotiwa kumuacha kiungo Kevin De Bruyne aamue mwenyewe hatima yake kama anataka kubaki au kuondoka.
Kiungo huyo wa Kibelgiji amebakiza miezi mitano kwenye mkataba wake na tayari amekuwa akihusishwa na klabu kibao za Saudi Arabia na Marekani zinazohitaji saini yake. De Bruyne amecheza mechi 23 msimu huu na aliwahi kufichua kwamba yupo tayari kuendelea kubaki Etihad.
De Bruyne, ambaye mkataba wake mpya aliosaini kwenye kikosi hicho ambao umemshuhudia akilipwa Pauni 385,000 kwa wiki utafika tamati mwishoni mwa msimu huu. Klabu kibao zinahitaji huduma ya mchezaji huyo, ikiwamo San Diego ya MLS, ambayo imekuwa ikifuatilia kwa karibu kabisa maendeleo ya kimkataba ya mchezaji huyo huko Etihad.
Wakati ukiwa hakuna mazungumzo yoyote rasmi, lakini Man City imemwaacha De Bruyne aamue hatima yake huku dirisha la usajili la majira haya ya baridi likifungwa kesho, Jumatatu.
STAA Mathys Tel ameripotiwa kwamba hajafuta mpango wa kubaki Bayern Munich hadi dirisha litakapofungwa baada ya kugomea ofa ya kwenda kukipiga Tottenham Hotspur. Spurs ilipeleka ofa kumsajili Tel kwa Pauni 50 milioni na ilielezwa Bayern ilikubali kabla ya mchezaji huyo kinda mwenye umri wa miaka 19 kugoma kwenda kujiunga na timu hiyo inayonolewa na Ange Postecoglou. Manchester United, Aston Villa, Arsenal na Chelsea nazo zinahitaji saini yake.
FULHAM imeripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili winga wa AS Roma, Matias Soule kwa mkopo kabla ya dirisha halijafungwa kesho, Jumatatu. Kocha Marco Silva anataka kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji baada ya Harry Wilson kuumia. Kutokana na Wilson kuumia na kutarajia kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, miamba hiyo ya Craven Cottage inahitaji saini ya mkopo ya Soule ili kuja kuongeza nguvu.
EVERTON imeripotiwa kuwa kwenye dakika za mwisho kumrudisha kiungo wa Kiargentina, Carlos Alcaraz kwenye Ligi Kuu England. Baada ya kutamba Southampton na Juventus, Alcaraz alihamia Flamengo mwaka jana. Na sasa ripoti zinafichua Everton ipo kwenye hatua za mwisho kumsajili ikiwa tayari kukubali dili la mkopo hadi mwisho wa msimu huku kukiwa na makubaliano ya kumchukua jumla.
LEICESTER City imeripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili beki wa Brighton, Tariq Lamptey kabla ya dirisha hili la majira ya baridi halijafungwa. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akiwekwa benchi huko Seagulls msimu huu, akicheza kwenye mechi tisa tu za Ligi Kuu England. Lamptey amefunga mara mbili na kuasisti mara mbili kwenye kikosi cha Brighton.
ASTON Villa inamtazama Joao Felix kama chaguo la kwanza la mchezaji wa kuchukua buti za Jhon Duran baada ya kujiunga na Al-Nassr. Kocha wa Aston Villa, Unai Emery amekuwa akihitaji saini ya Felix tangu dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, lakini Chelsea ilibaki naye. Na sasa likiwa dirisha la Januari likiwa wazi hadi kesho Jumatatu anataka kurudi tena kwa Felix.
CHELSEA imeripotiwa kwenda kumsajili straika wa Brighton, Evan Ferguson. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca anahitaji kuongeza straika kabla dirisha la usajili halijafungwa kesho. Ripoti zinafichua miamba hiyo ya Stamford Bridge imeingia kwenye vita ya kufukuzia huduma ya mchezaji huyo wa Jamhuri ya Ireland aongeze nguvu kufukuzia ubingwa Ligi Kuu England.
TOTTENHAM Hotspur imeripotiwa kufanya mazungumzo na Manchester United ili kunasa huduma ya winga Alejandro Garnacho. Spurs ilifanya mawasiliano na mabosi wa Man United juzi baada ya kushindwa kumsajili Mathys Tel wa Bayern Munich na sasa imepeleka maombi Man United kumchukua Garnacho kwa mkopo wa nusu msimu.