Cunha mambo freshi Manchester United

Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kila kitu kipo sawa na Manchester United imekubali kulipa ada ya Pauni 62.5 milioni ili kuipata saini ya mchezaji huyo ambaye amekuwa moto kwelikweli msimu huu.
MSHAMBULIAJI wa Wolvelvehamton Wolverhampton Wanderers na timu ya taifa ya Brazil, Matheus Cunha huenda akajiunga na Manchester United baada ya msimu huu kumalizika.
Kwa mujibu wa taarifa kila kitu kipo sawa na Manchester United imekubali kulipa ada ya Pauni 62.5 milioni ili kuipata saini ya mchezaji huyo ambaye amekuwa moto kwelikweli msimu huu.
Supastaa huyo mwenye umri wa miaka 25 amekubali kujiunga na Man United kutokana ma ushawishi mkubwa wa kocha wa timu hiyo, Ruben Amorim.
Cunha amekuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo atika kikosi cha Wolves kwa msimu huu ambapo amecheza mechi 34 za michuano yote na amefunga mabao 17 na kuasisti sita.
Mkataba wa sasa wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika ifikapo 2029. Mbali ya Man United saini yake pia inahitajiwa na vigogo wa Saudi Arabia.
Florian Wirtz
BAYER Leverkusen inadaiwa kutaka Pauni 126 milioni ili kumuuza staa wa kimataifa wa Ujerumani, Florian Wirtz, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mchezaji huyo anawindwa na vigogo mbalimbali Ulaya ikiwa pamoja na Bayern Munich na Liverpool. Awali, alionekana kuwa na nafasi kubwa ya kutua Manchester City, lakini taarifa zinaeleza kwamba matajiri hao wa Jiji la Manchester wamejitoa katika dili hilo.
Mason Greenwood
MARSEILLE imesisitiza kwamba haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Jamaica, Mason Greenwood, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Greenwood anahusishwa sana kuondoka katika dirisha lijalo baada ya kocha wa timu hiyo, Roberto de Zerbi kuweka wazi kwamba staa huyo anatakiwa kubadilika ikiwa anataka kupata nafasi zaidi.
Jeremie Frimpong
BEKI kisiki wa Bayer Leverkusen, Jeremie Frimpong, 24, anadaiwa kufanya vipimo vya afya Jumatatu kabla ya kukamilisha dili la kujiunga na Liverpool katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Liverpool inataka kumsajili Frimpong kwa ajili ya kuziba pengo la Trent Alexander Arnold ambaye anaondoka mwisho wa msimu huu kujiunga na Real Madrid.
Liam Delap
MANCHESTER United imefanya mazungumzo ya ana kwa ana na wawakilishi wa straika wa Ipswich Town na timu ya taifa ya England, Liam Delap, 22, katika harakati za kutaka kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Man United na baadhi ya timu kubwa za England zimeanza kupambania huduma yake tangu dirisha la majira ya baridi mwaka huu baada ya kiwango bora alichoonyesha.
Upamecano
MAZUNGUMZO kati ya wawakilishi wa Bayern Munich na beki wao wa kimataifa wa Ufaransa, Dayot Upamecano, 26, yameshaanza yakiwa na lengo la kufanikisha mchakato wa staa huyo kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuwatumikia hadi mwaka 2030. Upamecano ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Bayern na msimu huu alihusika kuisaidia kushinda Bundesliga.
Nuno Tavares
LAZIO inapanga kuongeza dau inalotaka kuilipa Arsenal katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ajili ya kumnunua mazima beki wa kushoto wa timu hiyo ambaye ni raia wa Ureno,Nuno Tavares. Mabosi wa Lazio wanataka kutoa kiasi hicho cha pesa baada ya ripoti ya kocha kusisitiza asajiliwe kwani ameridhishwa na kiwango ambapo anacheza kwa mkopo.
Caoimhin Kelleher
BASTON Villa inataka kumsajili kipa wa Liverpool na Jamhuri ya Ireland, Caoimhin Kelleher, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuziba pengo la kipa wa kimataifa wa Argentina, Emiliano Martinez, 32, anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu kwenda kusaka maisha kwengineko. Emiliano anadaiwa kutaka kuondoka na kujiunga na timu mojawapo ya Saudi Arabia.