Arsenal yapanga kukata rufaa
Muktasari:
- Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Arsenal kushinda bao 1-0, mwamuzi Michael Oliver alimtoa Lewis-Skelly mwenye umri wa miaka 18 nje ya uwanja muda mfupi kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza kwa kosa la kumchezea faulo Matt Doherty wakati Wolves ilipokuwa inaandaa shambulizi.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amesema timu hiyo itakata rufaa juu ya kadi nyekundu ya beki wao Myles Lewis-Skelly aliyoonyeshwa katika mchezo dhidi ya Wolves ikiwa FA haitaifuta.
Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Arsenal kushinda bao 1-0, mwamuzi Michael Oliver alimtoa Lewis-Skelly mwenye umri wa miaka 18 nje ya uwanja muda mfupi kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza kwa kosa la kumchezea faulo Matt Doherty wakati Wolves ilipokuwa inaandaa shambulizi.
Kadi hiyo ilisababisha wachezaji wa Arsenal kumzunguka mwamuzi Oliver kwa hasira wakionyeshwa kutokubaliana na uamuzi wake.
Awali, ilionekana kama Lewis-Skelly alionyeshwa kadi nyekundu kwa sababu alimzuia Matt kuanzissha shambulizi la kwenda kufunga bao lakini hilo lilikuwa linapingwa kwani mchezaji huyo alikuwa jirani zaidi na lango lake.
Hata hivyo, chombo kinachohusika na usimamizi wa waamuzi wa EPL, PGMOL kupitia ukurasa wake wa X, kilitoa ufafanuzi juu ya tukio hilo kikieleza kwamba lilitafsiriwa kama Skelly alicheza rafu hatari na baada Oliver kutoa uamuzi, mwamuzi wa VAR, Darren England aliidhinisha kadi hiyo.
Kutolewa nje kwa Lewis-Skelly kulikuwa tukio la nne kwa Arsenal msimu huu kwenye ligi. Wolves pia walipunguzwa na kubaki wachezaji 10 katika dakika ya 70 baada ya Joao Gomes kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano.
Arteta alisema: “Ni dhahiri kiasi kwamba nawaachia nyinyi kujadili.”
“Nimekasirika sana lakini nawaachia ninyi, kwa sababu ni inaonekana wazi sana. Sidhani kama maneno yangu yatasaidia kitu. Tunatumaini hatutofikia hatu ya kukata rufaa ingawa kama ikishindikana tutafanya hivyo, msimu huu kumekuwa na matukio kama haya, imewahi kutokea na kuna mfano mzuri kwa kile kilichotokea kwa Bruno (Fernandes). Kimsingi tuko katika nafasi ambayo hatupaswi kuwa.”
Bruno Fernandes wa Manchester United alitolewa nje dhidi ya Tottenham Septemba 29, 2024, lakini kadi yake nyekundu ilifutwa na FA baada ya rufaa kufanikiwa.