ZILITRENDI: Beki Yanga nusura atekwe na Simba
TAREHE kama ya leo, lakini mwaka 2004, beki wa Yanga kutoka Mbanga FC Kigoma, Ramadhan Rashid 'Carlos' alinusurika kutekwa na baadhi ya viongozi wa Simba.
Habari zilizotrendi kipindi hicho zilisema jaribio la viongozi hao kutaka kumteka mchezaji huyo na kumhamishia katika hoteli anayokaa sasa lilikwama baada ya Carlos kuwaacha kwenye mataa viongozi hao waliotaka apande gari lao wakamalizane.
Inadaiwa wakati wa usajili umekwisha Simba inamtaka mchezaji huyo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame iliyopfanyikia Kigali Rwanda kwani ni pasipoti tu ambayo hutakiwa kwenye mashindano hayo.
Tukio hilo linadaiwa ni mfululizo wa majaribio mawili ya kutaka kumteka na kumsainisha beki huyo aliyesajiliwa Yanga ili akazibe pengo la Ramadhan Wasso aliyejiunga na Yanga hivi karibuni ambapo hata hivyo muda wa usajili umekwisha.
Akizungumza na Mwanaspoti kipindi hicho, Carlos alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema amekuwa akifuatwa na viongozi wa Simba mara kwa mara wakimtaka kujiunga na klabu hiyo ili aikache Yanga.
Lakini alishindwa kuwataja majina ya viongozi hao kwa kudai hawajui kwa majina yao ila anawajua ni wa Simba.
"Walianza kunifuata katika hoteli ya Nanga ninakokaa siku moja kabla hawajaenda Zambia wakiniita nisaini Simba kwa ajili ya Kombe la Kagame halafu wanifiche lakini nikakataa wakasema timu ikirudi watanifuata."
"Alhamisi usiku baada ya kutoka kwenye msiba wa Kwela Mwaluvinga wakaja kunifuata tena wananiambia tutakupa mamilioni na vitu kibao ili nipande gari lao nikasaini mbele ya viongozi wengine nikatoroka nikawaacha wakishangaa," alisema Carlos.
Carlos alisema heri asicheze soka msimu mzima kuliko kuisaliti Yanga pamoja na Mkurugenzi wake Salum Luhuza wa Mbanga ambaye alifanikisha kumleta kwenye timu hiyo.
"Kwa hali hii siwezi kuisaliti Yanga na Luhuza heri nisicheze kabisa soka msimu mzima kuliko kudanganyika na mamilioni ya Simba ambayo yataniharibia maisha yangu mimi nina msimamo," alisema Carlos.
Habari za uhakika zinasema mchezaji huyo kupitia kwa rafiki wake wa karibu alitaka kupewa dau la sh 3milioni ili akubali kumwaga wino Simba kwa ajili ya kuichezea kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Hata hivyo, Carlos ametoa madai hayo ikiwa ni siku chache tangu Simba ilalamike kwa Chama cha Soka nchini (FAT), kwamba mchezaji huyo sio raia wa Tanzania.
"Wanahangaika tu si waende wakaulize uhamiaji kwani FAT, ndio inatoa uraia mimi kucheza Inter Stars ya Burundi sio kigezo cha kuwa Mrundi kwani nilikuwa natafuta maisha tu," alisema Carlos.
Wachezaji wengine wanaolalamikiwa ni Ramadhan Wasso, Wakongo Pitchou Kongo, Patrick Katalay na Alou Kuzulu Ziwanuka.
Viongozi wa Simba wamekanusha madai ya mchezaji huyo kwa madai hawawezi kufanya jambo kama hilo kwani muda wa usajili umekwisha.
Simba imekuwa ikikabiliwa na tatizo la namba tatu kutokana na kuhama kwa Wasso aliyekwenda kujiunga na Yanga.