Prime
Zamalek washusha mzigo Yanga

Muktasari:
- Rekodi ya kwanza ni kwamba anakwenda mchezaji wa kwanza wa Tanzania Bara kuuzwa kwa dau kubwa zaidi nje ya nchi, lakini pili anakuwa staa wa kwanza mzawa kununuliwa na Zamalek ndani ya miaka 20 iliyopita.
NDANI ya wiki chache zijazo, mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize ataweka rekodi mbili kwenye soka la Tanzania endapo dili lake la kucheza nje litakwenda kama lilivyopangwa.
Rekodi ya kwanza ni kwamba anakwenda mchezaji wa kwanza wa Tanzania Bara kuuzwa kwa dau kubwa zaidi nje ya nchi, lakini pili anakuwa staa wa kwanza mzawa kununuliwa na Zamalek ndani ya miaka 20 iliyopita.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya Mwanaspoti, dili lake la kujiunga na Zamalek liko kwenye hatua nzuri kutokana na makubaliano ya pande tatu kufikia pazuri.
Taarifa zinabainisha kuwa, Yanga imekubaliana na Zamalek ya Misri inayotaka kumsajili Mzize kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kufikia muafaka wa maslahi kwa pande hizo sambamba na uongozi unaomsimamia mchezaji anayehusishwa na klabu za Ufaransa na Morocco wiki kadhaa zilizopita.
Bosi mmoja wa juu kutoka Yanga, amefichua kuwa Zamalek imekubali kutoa Dola 750,000 (Sh2 bilioni) kumnunua mshambuliaji huyo aliyebakiza mkataba wa miaka miwili kikosini hapo.
Inaelezwa kwamba, Zamalek italipa fedha hizo kwa mafungu mawili ambapo kutakuwa na malipo yatakayofanyika kabla ya mchezaji huyo kuondoka kisha awamu ya pili yatafanyika Januari 2026 ambapo pande hizo mbili zimekubaliana.
Malipo ya kwanza ya mauzo hayo yatakayofanyika ni dola 375,000 (Sh991 milioni), kisha kiasi kama hicho kitalipwa baadaye kukamilisha makubaliano yaliyopo kufanya jumla kuwa ni dola 750,000.
Awali ilielezwa Mzize alikuwa na ofa nyingi za hukohuko Afrika Kaskazini kwa mataifa ya Morocco, Libya na hata Ulaya lakini Zamalek ndio ilikuwa kinara kwa kufikia makubaliano mazuri na Yanga.
“Mzize ni muda tu unahesabiwa, tulishakubaliana kila kitu ila ataondoka mwisho wa msimu ukimalizika hataweza kuondoka kama Aziz KI (Stephanie), na wao Zamalek walishakubaliana na hilo,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya Yanga.
“Kulikuwa na ofa nyingi lakini Zamalek ilikuwa na kitu tofauti zaidi kwa klabu na hata mchezaji, unajua hatutakiwi kuangalia maslahi ya klabu pekee na vijana wetu tunatakiwa kuwaangalia pia na ndiyo tulichofanya."
“Ukweli ni kwamba Mzize mwenyewe alikuwa na shauku sana ya kwenda kucheza Ulaya lakini kulikuwa na mambo ambayo yalikuwa magumu kukubaliana, kwahiyo hakuna namna atakwenda Zamalek na kila kitu kipo sawa."
Mzize amekuwa na wakati mzuri hasa msimu huu akiwa ndiye mshambuliaji mzawa kinara wa ufungaji katika Ligi Kuu Bara akifunga mabao 13 na asisti tatu huku akicheza mechi zote 27 kwa dakika 1,678.
Katika orodha ya wanaoongoza chati ya ufungaji, Mzize anashika nafasi ya pili akiwa sambamba na mshambuliaji mwenzake wa Yanga, Prince Dube, huku kinara ni kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua aliyefunga mabao 15.
REKODI ZA USAJILI BONGO
Kufikia sasa, mchezaji mzawa aliyenunuliwa kwa pesa nyingi moja kwa moja kutoka katika klabu ya Tanzania kwenda nje ni Mbwana Samatta, ambaye TP Mazembe ya DR Congo ililipa dola 100,000 (sawa na Sh250 milioni) ilipomnasa kutoka Simba 2011.
Baadaye Samatta aliuzwa kwa Euro 800,000 (sawa na Sh2.1 bilioni) mwaka 2016 kwenda KRC Genk ya Ubelgiji, ambako pia akaja kuuzwa Januari 2020 kwenda Aston Villa ya Ligi Kuu England kwa Euro 10 milioni (sawa na Sh26 bilioni).
Clatous Chama
Kwa wachezaji wa kigeni, Clatous Chama aliuzwa na Simba kwa Dola 300,000 (sawa na Sh793 milioni) kwenda RS Berkane ya Morocco mwaka 2022 kabla ya baadaye kurejea Msimbazi na kisha kutua Yanga alipo sasa.
Luis Miquissone
Raia huyu wa Msumbiji, aliuzwa na Simba kwenda kwa Mabingwa mara 12 wa Afrika, Al Ahly ya Misri mwaka 2021 kwa ada ya uhamisho ya dola 900,000 (sawa na Sh2.3 bilioni) kabla ya kurejea Simba 2023 ambako kisha alitemwa.
Fiston Mayele
Straika wa mabao kutoka DR Congo, alihama kutoka Yanga SC ya Tanzania kwenda Pyramids FC ya Misri kwa ada ya uhamisho ambayo haikutajwa hadharani lakini ikisemekana kuwa ni dola 900,000 (sawa na Sh2.3 bilioni).
Aziz KI
Kiungo raia wa Burkina Faso, hivi karibuni ametua Wydad ya Morocco akitokea Yanga kwa uhamisho uliogharimu Sh2.9 bilioni.