Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yule refa wa Simba, Berkane kumbe ndo zake

Muktasari:

  • Mwamuzi huyo analalamikiwa kuikandamiza Simba kutokana na kutotenda haki hali inayodaiwa imechangia kushindwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo baada ya sare ya 1-1 iliyofanya matokeo ya jumla kuwa RS Berkane 3-1 Simba kufuatia mechi ya kwanza iliyochezwa Morocco wenyeji kushinda 2-0.

KILICHOTOKEA kwa mwamuzi wa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba dhidi ya RS Berkane, Dahane Beida raia wa Mauritania, kinatajwa kuwa ni mwendelezo wa upepo mbaya alionao kwa timu za Tanzania huku baadhi ya uamuzi wa matukio uwanjani yakitafsiriwa si ya haki.

Mwamuzi huyo analalamikiwa kuikandamiza Simba kutokana na kutotenda haki hali inayodaiwa imechangia kushindwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo baada ya sare ya 1-1 iliyofanya matokeo ya jumla kuwa RS Berkane 3-1 Simba kufuatia mechi ya kwanza iliyochezwa Morocco wenyeji kushinda 2-0.

Matukio mawili makubwa ambayo yamewafanya mashabiki wa Simba kuwa na hasira ni kitendo cha kiungo wa timu hiyo, Yusuph Kagoma kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu dakika ya 50 kufuatia kuonyesha kadi mbili za njano. Pia bao alilofunga mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala dakika ya 77, iliamuliwa na VAR kwamba mfungaji alikuwa ameotea.

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' amesema: "Mwamuzi ametuumiza sana, mchezo ulikuwa wazi, hii ni fainali na uona kabisa kuna kadi imetoka iliyotufanya tuwe nyuma, kwa hiyo mwamuzi ameharibu fainali, lakini kwa upande wetu tulijiandaa vizuri na mechi tulishaikamata, tulikuwa tunaamini tunaweza kusawazisha na kupata ushindi."

Naye kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma, amesema: "Nafikiri mwamuzi aliimaliza ile mechi, tulijiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunapata ushindi kwenye mchezo ule na tunatwaa ubingwa.

"Hatukucheza muda unaotakiwa, nafikiri kama ni dakika nyingi sana basi tumecheza dakika 66 tu za muda wote kwenye mchezo huu.

"Maamuzi ya mwamuzi wa kati yaliathiri kwa kiasi kikubwa mchezo huu, lakini kwa ujumla tunapenda kuwapongeza Berkane kwa kutwaa ubingwa huo.

Wakati huohuo, nyota wa zamani wa Simba, Dua Said amesema ingekuwa ni mtu mmoja ambaye analalamika kuhusu mwamuzi ingeonekana sio sawa, lakini ni wengi, hivyo maana yake ukweli kuwa hakufanya sawa.

"Watu walianza kuongea kabla ya mechi kuanza kuhusu mwamuzi, inaonekana kabisa alikuja kwa maelekezo maalum," amesema mkongwe huyo.

Rekodi zinaonyesha mwamuzi huyo amechezesha mechi 26 za michuano ya CAF ngazi ya klabu tangu 2019, huku akiwa ameonyesha kadi za njano 103 na nyekundu nne. Pia ametoa penalti saba.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa mwamuzi huyo kuchezesha mechi ya Simba baada ya ile ya robo fainali ya African Football League dhidi ya Al Ahly iliyomalizika kwa sare ya 2-2, Oktoba 20, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Katika mechi zote mbili, Simba imetoka sare, haijashinda wala kupoteza.

Wakati Simba ikimlalamikia mwamuzi huyo, pia anakumbukwa kwa tukio la Aprili 5, 2024 lililozua gumzo baada ya shuti la Stephane Aziz Ki alilopiga dakika ya 58 dhidi ya Mamelodi Sundowns waliokuwa wenyeji wa mechi ya pili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Afrika Kusini, kwani licha ya mpira kuonekana kudundia ndani, lakini alikataa bao baada ya kwenda kujiridhisha kwenye VAR.

Mechi hiyo ilimalizika kwa matokeo ya 0-0 baada ya awali kushindwa kufunga pia jijini Dar es Salaam na kuamuliwa zipigwe penalti na Yanga ikapoteza kwa mikwaju 3-2.

Mwamuzi huyo pia alichezesha fainali ya mkondo wa pili Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya USM Alger ugenini iliyochezwa Juni 3, 2023. Licha ya Yanga kushinda, lakini haikubeba kombe kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2, ikahukumiwa na bao la ugenini kufuatia nyumbani kufungwa 2-1.

Katika kazi ya urefa, Dahane Beida alianza kuchezesha mashindano ya CAF msimu wa 2018/19 katika Kombe la Shirikisho, kisha AFCON U-17 mwaka 2019 iliyofanyika nchini Tanzania. Hadi sasa, mwamuzi huyo amechezesha mechi 14 za Ligi ya Mabingwa, huku Kombe la Shirikisho zikiwa 10.

Mashindano mengine ya CAF aliyochezesha ni Kufuzu AFCON (8), AFCON (5), AFCON U-17 (2), CHAN (2) na African Football League (1).