Yanga: Msitufokee... kama vipi njooni Kigoma

Muktasari:

  • YANGA imesikia kelele za mashabiki wa Simba baada ya jana kukabidhiwa taji lao la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo, kisha wakaambiwa ‘mtufokee na kama vipi tukutane Kigoma’, huku mabosi wao timu hiyo wakipanga, wakishamaliza kuua mnyama tu, timu iende kambini Morocco.

YANGA imesikia kelele za mashabiki wa Simba baada ya jana kukabidhiwa taji lao la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo, kisha wakaambiwa ‘mtufokee na kama vipi tukutane Kigoma’, huku mabosi wao timu hiyo wakipanga, wakishamaliza kuua mnyama tu, timu iende kambini Morocco.

Watani hao, watakutana Kigoma katika fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) pambano litakalopigwa wikiendi hii, huku timu zote zikitambiana, Wekundu wakiwakejeli Yanga kwamba wanashangilia ushindi wao wa derby, lakini wao wanabeba makombe na watawaonyesha Jumapili.

Hata hivyo, mashabiki wa Yanga wamejibu mpigo wakidai kuwa, Lake Tanganyika moto utawaka kwani wamepania kushinda na kubeba ubingwa wa ASFC, kisha baada ya hapo watasepa zao Morocco kuweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi vijiweni ni kelele juu ya Simba kubeba ndoo na mazagazaga yake, lakini kitu cha ajabu pamoja na uimara wao wote wameshindwa kuifunga Yanga, huku wakikumbushwa kuwa Jumapili hii kama hawatakaa vizuri watapigwa tena na Jangwani.

Mchezo huo wa fainali ya ASFC ni wa nne kati ya timu hizo msimu huu, baada ya awali kukutana mara mbili katika Ligi Kuu Bara, huku Yanga ikishinda mechi moja na kupata sare, kadhalika kuichapa tena Simba kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021.

Hata hivyo, hiyo ni mechi ya pili kwa timu hizo kukutana ndani ya misimu miwili ya ASFC, kwani msimu uliopita walivaana katika nusu fainali na Simba kuishindilia Yanga mabao 4-1, kitu kinachofanya mashabiki wake kuamini hata Jumapili inaweza kuendelea ubabe kwa watani wao.

Nyota wa Yanga wameungana na mashabiki wao, wakisisitiza kuwa, wamemaliza Ligi na sasa akili zao ni kwenye mchezo huo ili kuwanyoosha watani wao na kubeba ubingwa huo baada ya kukosa lile la Ligi Kuu Bara.

Feisal Salum na nahodha wake msaidizi, Bakar Mwamnyeto na hata Msemaji wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli walikaririwa na Mwanaspoti kuwa, Kigoma lazima kieleweke kwani wanataka kumaliza msimu kwa heshima kubwa.

KAMBI MOROCCO

Licha ya kupigia hesabu fainali ya ASFC, mabosi wa Yanga pia wamepania msimu ujao kuja kwa kasi sana wakifanya usajili, lakini wanaangalia watatoka vipi kwa msimu unaokuja na sasa kuna mpango flani wa kwenda Uarabuni kujiandaa na msimu.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi alitaka kuipeleka timu kambini Ulaya kule Uturuki, kambi ambayo waliwahi kwenda miaka ya nyuma tena mara mbili tofauti enzi za Yusuf Manji, hata hivyo safari hiyo haitaweza kufanyika tena kutokana na sheria kadhaa dhidi ya janga la corona.

Lakini mabosi wake, fasta wakapata akili ya kwenda kuiweka timu nchini Morocco na tayari mchakato wa kambi hiyo umeshaanza.

Yanga itaweka kambi ya wiki kadhaa nchini humo kujiandaa na msimu ujao na mchakato wake umeshakaa sawa baada ya safari ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said.

Hersi anayerejea leo nchini alikuwa Morocco kwa mualiko wa klabu ya Raja Casablanca walioingia nao makubaliano ya ushirikiano kati ya klabu hizo mbili.

Mbali na kwenda kuonana na mabosi wa Raja pia juzi Hersi alikuwa katika Uwanja wa Mohamed V, akiishuhudia Al Ahly ikichukua taji lake la 10 la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga Kaizer Chiefs kwa mabao 3-0.