Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga inachapa tu, Okello hashikiki

Muktasari:

  • Katika harakati hizo, leo imefanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo, mechi ikichezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam na kukaa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 60.

KWA sasa Yanga inachofanya ni kushinda mechi zake ili kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara katika harakati za kuteteta ubingwa wao iliouchukua misimu minne mfululizo huku kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Allan Okello akiwa hashikiki.

Katika harakati hizo, leo imefanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo, mechi ikichezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam na kukaa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 60.

Wakati Yanga hali ikiwa hivyo, Namungo inazidi kudidimia, huku ikiwa haijapata ushindi katika mechi 16 mfululizo za mashindano tofauti tangu mara ya mwisho ishinde 1-0 dhidi ya KMC ambapo kabla ya hapo, pia ilizifunga Coastal Union (1-0), Mbeya City (1-0) na Dodoma Jiji (2-0).

Tangu hapo, Namungo imepata sare saba, ikipoteza tisa ikiwemo moja ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA United.

Katika mechi ya leo, Yanga ndio ilitawala kipindi cha kwanza ikionekana kutengeneza mashambulizi ya kuufungua ukuta mgumu wa Namungo walioamua kulinda zaidi lango kuliko kushambulia.

Yanga ilifanikiwa kupata bao la Kuongoza dakika ya 26, mfungaji akiwa kiungo Duke Abuya wakati wenyeji wakifanya shambulizi la haraka na mfungaji kukimbia umbali mrefu akifanikiwa kupita katikati ya mabeki, akauweka kambani mpira.

Bao hilo lilipatikana baada ya Yanga kupiga pasi tatu kuanzia kwa Mohamed Damaro ambaye alipokonya mpira, kisha kutoa pasi kwa Allan Okello naye kumpa Mudathir Yahaya aliyemuwekea mfungaji aliyekimbia na kuwatoka wachezaji wa Namungo na kwenda kufunga.

Namungo ikafanya shambulizi moja tu wakifika kwa mara ya kwanza lango la Yanga ikafanikiwa kupata bao dakika ya 40, mfungaji akiwa Salum Kabunda akimalizia krosi ndefu ya beki wa kulia, Bakari Hussein.

Bao hilo linakuwa la pili mfululizo kwa Kabunda ambaye kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, alifunga ikiwa ni sare ya bao 1-1.

Bao hilo ilikuwa kama inairudisha Yanga kuona kipa wake Djigui Diara anaruhusu kwenye ukuta wanaocheza mabeki wake Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Abdulla 'Bacca'.

Mchezo uliopita ambao Yanga ilishinda nyumbani kwa mabao 3-0 na hata ule wa Kombe la Shirikisho la CRDB ambao kipa huyo alicheza sambamba na mabeki wa kati Frank Assinki na Bacca, hawakuruhusu bao. Kabla ya hapo, aliruhusu wakati Yanga ikifungwa 3-2 na Dodoma Jiji.

Kipindi cha kwanza cha mechi hiyo kilikuwa sare ya bao 1-1, hali iliyofanya benchi la ufundi la Yanga linaloongozwa na Abdihamid Moallin akishirikiana na Patrick Mabedi kwenda mapumziko kujiuliza.

Kwa upande wa Namungo, Kocha Juma Mgunda na wenzake wa benchi la ufundi, nao walienda kujipanga vyumbani wakitarajia kurudi kwa namna nyingine kuhakikisha wanapambana kuondoka na pointi.

Kipindi cha pili Yanga ilirudi na mabadiliko ikimtoa kiungo mkabaji Damaro, nafasi yake ikichukuliwa na Edmund John.

Mabadiliko hayo yalibadili muundo wa Yanga ikimrudisha chini Mudathir huku Edmund akienda kucheza kiungo akishambulia akitokea pembeni, wenyeji wakilenga kuongeza kasi ya ushambuliaji.

Yanga ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53, mfungaji akiwa Okello akiuwahi mpira wa krosi ya Dube uliochelewa kuokolewa na beki wa Namungo Abdallah Mfuko.

Bao hilo Namungo itajilaumu yenyewe baada ya kupoteza mpira eneo la hatari, nahodha wake Jacob Massawe pasi yake ya kurudisha nyuma ikanaswa na Dube, kisha kuweka pasi ya ndani ikaenda kutumiwa na Okello.

Bao hilo lilikuwa la 10 kwa Okello akifunga kwenye mechi tatu mfululizo za ligi, akiendelea kuonyesha makali huku akiibeba Yanga aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2026.

Okello akaongeza la tatu dakika ya 85 na la 11 kwake akimfukuza kwa ukaribu kinara Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam mwenye 12 kabla hajacheza dhidi ya KMC.