Wanigeria wa Yanga presha tupu, kutua leo
WAPINZANI wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Rivers United kuanzia leo watatua nchini muda wowote kwa mchezo wao wa raundi ya wali, huku wakiifuatilia Yanga kimyakimya na kujua wanakuja kucheza na timu isiyo ya mchezomchezo na fasta wameamua kukuna kichwa ili wasije wakaaibika.
Rivers watavaana na Yanga Jumapili hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kurudiana nao katika mchezo wa kuamua nani avuke kuingia raundi ya kwanza Septemba 19, mechi itakayopigwa katika Uwanja wa Adokiye Amiesimaka uliopo mjini Port Harcourt.
Hata hivyo, Rivers wameanza kuingia ubaridi baada ya kutafuta mechi za chapchapu dhidi ya majirani zao Bayelsa United ili kuwapa utimamu kabla ya kuja Dar es Salaam kuvaana na Yanga ambao jana ilikuwa ikivaana na Pan Africans na leo ikamalizana na KMC katika mechi za kirafiki za kutesti mitambo.
Katika mechi yao ya awali iliyopigwa Alhamisi, Rivers na Bayelsa iliisha kwa sare ya 1-1 na jana jioni walikuwa wakirudiana kwenye Uwanja wa Samson Siasia mjini Yenagoa, huku Ofisa Habari wa timu hiyo ya Nigeria, Charles Mayuku akisema wanatafuta mechi nyingine ya mwisho kabla ya kuja Dar.
Yanga na Rivers litachezeshwa na Mwamuzi, Hassan Mohamed Hagi kutoka Somalia, akisaidiwa Suleiman Bashir Abdi na Ali Mohamud Mahad na wa akiba atakuwa Ahmed Hassan Hussein wote wakitokea pia Somalia na Kamisaa atakuwa Lewis Blaze Madeleine kutoka Seychelles.
Hii ni mara ya kwanza wa timu hizo kukutana katika mechi za kimataifa, japo Yanga ina rekodi ya kukutana mara kadhaa wa Wanigeria na kutaabika ikiwamo dhidi ya Enugu Rangers na Kwara United.