Walibya waichelewesha KMKM
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeahirisha mchezo wa Kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya KMKM na Al-Itthad ya Libya uliokuwa uchezwe leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja na badala yake sasa utachezwa kesho Jumapili kuanzia saa 8:00 mchana.
Akitoa taarifa jioni hii ya kuahirishwa kwa mchezo huo, Mratibu wa Masuala ya Kimataifa ndani ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mbarouk Othman alisema mchezo huo umeahirishwa kutokana na tatizo la usafiri lililowapata Al-Itthad hadi kufika visiwani Zanzibar.
"Sababu kubwa ya kuahirishwa kwa mchezo huu CAF walitutumia taarifa kwenye barua pepe yetu ya shirikisho kutokana na changamoto ambazo Al-Itthad wamezipata ikiwemo vibali vya kupita katika Air Space, kwa mujibu wa barua pepe ilikuwa ngumu kupata vibali, hivyo kusababisha kuchelewa kufika Zanzibar na CAF walisema itakuwa ngumu kupata matokeo ya Uviko-19 kwa muda sahihi," alisema.
Kwa upande wao KMKM kupitia kocha msaidizi, Ame Msimu Khamis alisema kuahirishwa kwa mchezo huo kumewaathiri kwa kiasi fulani, ila watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na hivyo kusonga hatua nyengine.
"Imetuathiri sana sasa tunaenda kukaa na wachezaji ili warudisha morali yao kama waliyokuwa nayo maana tulijapanga kucheza leo, lakini CAF ndo wenye mamlaka hivyo tutaongea nao wachezaji na tutajipanga tena kwa ajili ya kesho," alisema.
Kutokana na badiliko hilo, CAF imeamua mechi ya KMKM na Al Ittihad ipigwe saa 8 mchana na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Mafunzo na GD Interclube ya Angola itafuatia saa 10:15 jioni kwenye uwanja huo huo wa Amaan.
IMEANDIKWA NA MOSI ABDALLA, UNGUJA