Vuzurugu za mashabiki MC Alger zazua taharuki Amaan Complex
Muktasari:
- Tukio hilo lilianza majira ya saa 7:30 mchana, ambapo kundi la mashabiki wa timu hiyo lilionekana kutoridhishwa na utaratibu uliowekwa wa kuingia uwanjani, hali iliyosababisha mvutano kati yao na maofisa waliokuwa wakisimamia uingiaji wa watazamaji.
Vurugu zimezuka katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, baada ya kundi kubwa la mashabiki wa MC Alger ya Algeria kukabiliana na maofisa wa usalama, wakiwemo maofisa wa polisi na walinzi, katika eneo la kuingilia jukwaa la Urusi kwenye uwanja huo.
Tukio hilo lilianza majira ya saa 7:30 mchana, ambapo kundi la mashabiki wa timu hiyo lilionekana kutoridhishwa na utaratibu uliowekwa wa kuingia uwanjani, hali iliyosababisha mvutano kati yao na maofisa waliokuwa wakisimamia uingiaji wa watazamaji.
Mvutano huo uligeuka kuwa vurugu katika lango la kuingilia jukwaani hapo huku baadhi ya mashabiki wakionekana kusukumana na kukabiliana na walinzi pamoja na polisi waliokuwa wakijaribu kudhibiti hali hiyo.
Katika purukushani hizo, baadhi ya maofisa wa usalama walionekana kupata majeraha baada ya kushambuliwa na vitu vyenye ncha kali. Mmoja wao alishuhudiwa akiondolewa eneo la tukio akiwa na jeraha kichwani lililosababisha kuvuja damu.
Vurugu hizo ziliendelea kwa takribani dakika 10 kabla ya hali kutulia na mashabiki hao kuruhusiwa kuingia uwanjani. Hata hivyo, utulivu huo haukudumu kwa muda mrefu, kwani baada ya dakika 20 tangu kuingia kwao, vurugu nyingine zilizuka katika eneo walilokuwa wamekaa.
Katika tukio hilo la pili, baadhi ya walinzi waliokuwa wakisimamia eneo hilo walionekana kukimbia huku hali ya sintofahamu ikitawala katika sehemu ya jukwaa lililokuwa na mashabiki hao
Hali hiyo ililazimu baadhi ya maofisa wa MC Alger kwenda moja kwa moja katika eneo la mashabiki wao kuzungumza nao na kujaribu kurejesha utulivu huku muda ukiwa umesalia mchache kabla ya kikosi cha timu hiyo kuingia uwanjani.
Maofisa hao walituliza hali hiyo, wakati ambapo wachezaji wa MC Alger walikuwa wanajiandaa kuingia uwanjani kwa ajili ya kukagua mazingira ya uwanja kabla ya kuanza kupasha misuli.