Vodacom Coastal Classic yaunganisha michezo, utalii na maendeleo ya vijana Africa
Muktasari:
- Kagimu alitwaa ushindi wa wanaume akifuatiwa na Jordan Schleck, huku Ngwata akimaliza wa tatu. Kwa wanawake, Aleper alishinda akifuatiwa na Sitona Munu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku Mercy Elegay wa Kenya akishika nafasi ya tatu.
Waendesha baiskeli kutoka Uganda, Charles Kagimu na Mary Aleper, wametawala mashindano ya Vodacom Coastal Classic 2026 yaliyofanyika jana, huku Mtanzania Boniface Ngwata akishika nafasi ya tatu katika kundi la wanaume.
Kagimu alitwaa ushindi wa wanaume akifuatiwa na Jordan Schleck, huku Ngwata akimaliza wa tatu. Kwa wanawake, Aleper alishinda akifuatiwa na Sitona Munu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku Mercy Elegay wa Kenya akishika nafasi ya tatu.
Kagimu na Aleper kila mmoja alizawadiwa Sh10 milioni, washindi wa pili Sh7 milioni na waliomaliza wa tatu Sh3 milioni. Waendesha baiskeli waliomaliza nafasi ya nne hadi ya 10 walipata Sh1 milioni kila mmoja.
Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanaume Charles Kagimu kutoka Uganda (katikati) mshindi wa pili Jordan Schleck kutoka Uganda (kushoto) na mshindi wa tatu Boniphace Ngwata kutoka Tanzania (kulia), wakionesha mfano wa hundi walizokabidhiwa katika mashindano hayo. Washindi hao walijishindia milioni 10 kwa mshindi wa kwanza, milioni 7 kwa mshindi wa pili, na milioni 5 kwa mshindi wa tatu mtawalia.
Jumla ya waendesha baiskeli 147 walishiriki mbio hizo za kilomita 109 zilizoanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, na kumalizikia Bagamoyo.
Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania, Nguvu Kamando, aliwapongeza washindi na washiriki, akisema mashindano hayo yanatoa fursa kwa waendesha baiskeli kukuza vipaji vyao na kuchangia maendeleo ya jamii.
Washindani wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic wakiwa katika eneo la kuanzia mashindano hayo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kuelekea Bagamoyo, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Tehama wa Vodacom Tanzania Plc Athumani Mlinga
“Mbali na ushindani wenyewe, Vodacom Coastal Classic na Nyerere Cycling Tour vinasaidia kukuza utalii wa ndani, kusaidia mipango ya elimu na kuleta matokeo chanya kwa jamii zinazopatikana katika njia ya mashindano,” alisema Kamando.
Alisema mpango huo pia unalenga kuwawezesha vijana, wakiwemo wasichana, kutumia michezo kukuza vipaji na kujenga fursa za kiuchumi.
Mgeni rasmi na Afisa Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, aliwapongeza waandaaji na wadau kwa kutumia michezo kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kukuza utalii wa michezo.
Washiriki wa Mashindano ya Nyerere Cycling Tour wakiendelea na Mashindano hayo ukanda wa Pwani wa bahari ya Hindi kuelekea Bagamoyo
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ramadhani Rashid Katanga, alisema mashindano hayo yanaonesha nafasi inayoongezeka ya baiskeli katika kuhamasisha maisha yenye afya, kukuza vipaji vya vijana na kuibua fursa za kiuchumi.
Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, alisema mpango huo ni zaidi ya mashindano kwa kuwaunganisha waendesha baiskeli na jamii na kuenzi urithi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando (kushoto), akikabidhi tuzo kwa mshindi wa kwanza wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanawake, Mary Aleper (katikati) kutoka Uganda. Washindi wengine wa mashindano hayo walikuwa Ditona Munu Martinie mshindi wa pili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) (wa pili kushoto) na Mercy Elegae kutoka Kenya, aliyeshika nafasi ya tatu.
Vodacom Coastal Classic ni sehemu ya shughuli za Nyerere Cycling Tour, ambayo inaanza leo kwa safari ya kilomita 1,500 kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, itakayofanyika hadi Oktoba 14.
Ziara hiyo itahusisha waendesha baiskeli kutoka Tanzania na nchi nyingine na itaambatana na shughuli za elimu, afya, utalii na uhifadhi wa mazingira katika maeneo itakayopita.
Vodacom Tanzania ndiyo mshirika mkuu wa Nyerere Cycling Tour, ikisaidiwa na Afro Oil, Stanbic Bank Tanzania, DYD, ABC, Coca-Cola na Huawei.