Tupac: Kitanzi balaa la usupastaa na kashfa za kimapenzi
Muktasari:
Huyo ndiye Russell, ambaye kuna wakati Bongo alivumishwa kuwa na uhusiano wa kimalovee na mwanamitindo wa Bongo, anayetusua unyamwezini, Flaviana Matata
Katika sehemu zilizopita tuliona jinsi watu maarufu akiwamo mwandishi gwiji wa mashairi na kurekodi muziki, Russell Simmons, alivyoingia matatani akituhumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia. Leo
Staa wa Hollywood, Christina Moore, mwaka 2014, alisajili manung’uniko yake kupitia gazeti la The New York Times kuhusu Russell, kwamba siku moja alikuwepo maeneo ya kula bata, Soho Beach House, Miami.
Moore alisema kuwa ndani ya Soho Beach House, Russell alikuwa amechukua apartment. Alisema kuwa alikuwa hajui vizuri maeneo ya eneo hilo, hivyo akamuona Russell akiwa na wasaidizi wake, akamfuata kumuuliza ilipo bar.
Kwa mujibu wa Moore, badala ya Russell kumweleza baa ilipo, alimpa maelekezo ya kuingia kwenye apartment ya Russell, akamdanganya ndiyo baa. Moore alisema kuwa alishangaa kujikuta yupo ndani ya apartment ya Russell, na ghafla staa huyo alimvamia na kumlazimisha kushiriki naye mapenzi kwa nguvu.
Moore alisema kuwa kilichomwokoa ni kwamba siku hiyo alikuwa na watu wengine pale Soho Beach House. Anachoamini ni kwamba angekuwa peke yake, Russell angeweza kutimiza azma yake ya kumbaka kwa kusaidiwa na wasaidizi wake, maana tayari alishaingia chumbani.
Pamoja na kuponea chupuchupu kubakwa, Moore alisema kuwa kila anapokumbuka tukio hilo hujihisi kuvunjiwa heshima kwa kiasi kubwa, maana Russell alimshika maeneo ambayo kwake ni ya faragha, halafu bila ridhaa yake.
Kutokana na skendo mfululizo za unyanyasaji wa kingono kwa wanawake zinazomkabili Russell, mtangazaji tajiri, Oprah Winfrey, alilazimika kukifanyia uhariri kitabu chake, The Wisdom of Sunday, ili kuondoa nukuu zote za ushauri kutoka kwa Russell. Alifanya hivyo kwa kuona kwamba Russell si alama njema kwa jamii.
Huyo ndiye Russell, ambaye kuna wakati Bongo alivumishwa kuwa na uhusiano wa kimalovee na mwanamitindo wa Bongo, anayetusua unyamwezini, Flaviana Matata. Hata hivyo, Flavi alichomoa mbavuni kuwa yeye na Russell siyo siyo mabesti kimapenzi, ila ni mabesti kikazi.
Russell mbunifu wa mitindo ya mavazi, Flavi mwanamitindo. Hivyo kuwa karibu ilikuwa mwake kabisa. Hata hivyo, longtime Flavi na Russell hawaonekani karibu kama ilivyokuwa zamani.
Ukipitia mfululizo wa tuhuma za Russell, unaweza kushangaa kwa nini mpaka leo bado anadunda. Unapaswa pia kutambua kwamba hata Cosby, naye yalisemwa mengi, akawa anakanusha hata kudhaniwa anaogopwa, ila leo yupo jela. R Kelly pia alivuka vizingiti vingi, lakini kwa sasa anakabiliwa na mashitaka makubwa ya unyanyasaji wa kingono kwa mabinti wadogo.
TUPAC KAMA SOGGY
Desemba 1994, Rapa Tupac Shakur alihukumiwa kifungo jela kuanzia mwaka mmoja na nusu mpaka minne na nusu. Kosa likiwa kumnyanyasa kingono mwanamke mkazi wa Brooklyn, New York, Marekani.
Kesi hiyo ilitokana na tukio la Novemba 19, 1993, mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 19, alidai kuwa alimwamini Tupac kwa sababu ya umaarufu wake, hivyo aliingia naye chumbani kwenye Hoteli ya Le Parker Meridien, New York, lakini wakiwa ndani alimgeuzia kibao na kumnyanyasa kingono.
Tupac alijitetea kuwa mwanamke huyo akiwa na wenzake, walimvamia chumbani na kutaka kumuibia, alipowakabili ndipo walimfungulia mashitaka ya usumbufu wa kingono. Pamoja na utetezi huo Tupac alihukumiwa kifungo jela, ingawa aliachiwa miezi tisa baadaye kwa dhamana ya dola 1.4 milioni, sawa na Sh3 bilioni kwa sarafu ya sasa.
Aliyekuwa CEO wa studio za Death Row Records, Suge Knight, ndiye alilipa fedha hizo na kumtoa jela kwa makubaliano kuwa Pac angerekodi albamu tatu chini ya Death Row. Mwaka 2017 katika usiku wa kumtunuku Tupac tuzo ya Rock & Roll Hall of Fame, rapa Snoop Dogg alisimulia kwamba yeye ndiye alimshawishi Suge kumtoa jela Tupac.
Tupac kukutwa na hatia ya kesi ya ubakaji ilikuwa mshangao. Maana mwaka 1993 ndipo albamu ya Tupac, “Strictly 4 My N.I.G.G.A.Z” ilikuwa inabamba na wimbo kinara ulikuwa “Keep Ya Head Up”.
Katika wimbo Keep Ya Head Up, Tupac anatetea wanawake na vitendo vya ubakaji. Anawaonya black Americans kuacha tabia ya kuwanyanyasa wanawake, kuwabaka, kuwapiga na kadhalika. Umebaki kuwa wimbo wa Tupac unaotumika zaidi katika harakati za wanawake. Ni wimbo pendwa sana kwa wanawake.
Katika albamu ya kwanza ya Tupac, “2Pacalypse Now”, kuna wimbo mwingine kipenzi cha wanawake, unaitwa “Brenda’s Got a Baby”, unaozungumzia tatizo la mabinti wadogo kupewa mimba na kutelekezwa. “Brenda’s Got a Baby” ni stori ya binti mwenye umri wa miaka 12, aliyejifungua na kutupa mtoto kwenye pipa la takataka baada ya kuona hana msaada.