Prime
Tisa wazitesa Simba, Yanga
IDADI ya makocha waliofundisha Ligi Kuu Bara msimu huu 2025-2026 imezidi kuongezeka na sasa imefikia 39, hiyo ni baada ya Yanga kuachana na Pedro Goncalves, kisha kutangaza timu kuwa chini ya Abdihamid Moalin na Patrick Mabedi.
Katika kundi hilo la makocha 39, wapo walioondoka kabla ya Ligi Kuu kuanza lakini walishiriki katika maandalizi ya msimu huu, wapo waliohudumu kwa kukaimu nafasi katika muda mfupi, kuna waliopewa mikataba ya muda mrefu ikavunjwa lakini kuna ambao wanaendelea kuzitumikia timu zao hadi sasa.
Timu kongwe za Simba na Yanga zimeingia kwenye orodha ya kufundishwa na makocha wengi na jumla yake ni tisa. Yanga imenolewa na makocha wanne, wakati Simba ikiweka rekodi ya watano.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga na Simba ambazo zipo nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, chini yake Azam na JKT Tanzania zimekomaa na makocha wao hadi sasa.
Florent Ibenge aliyetua msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan, ameendelea kuinoa timu hiyo iliyopo nafasi ya tatu baada ya mechi 21 kabla ya kukabiliana na TRA United, ikiwa imekusanya pointi 43.
JKT Tanzania inayoshika nafasi ya nne na pointi 32 baada ya mechi 21, nayo imekomaa na Ahmed Ally ambaye yupo hapo tangu msimu uliopita akiwa ndiye kocha aliyedumu muda mrefu zaidi ndani ya ligi hiyo kwa sasa waliopo.
Kocha mwingine ambaye amebaki na chama lake hakuna mabadiliko ya benchi la ufundi ni Juma Mgunda wa Namungo aliyetua hapo msimu uliopita 2024-2025. Kikosi hicho kinapambana kujiweka salama kikiwa nafasi ya kumi na pointi 23 kabla ya mechi za raundi ya 22.
Pamba Jiji iliyo na pointi 29 nafasi ya saba kabla ya kuchezwa raundi ya 22, nayo haijafanya mabadiliko ya benchi la ufundi tangu kuanza kwa msimu huu ilipomtambulisha Francis Baraza.
Kuna sababu nyingi za timu kufanya mabadiliko ya mabenchi ya ufundi, lakini unapoona timu inashika nafasi ya kwanza au ya pili kwenye msimamo nayo inafanya hivyo, bila shaka kutakuwa na maswali ya kujiuliza.
Ishu ya Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 51 kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi hali iliyofanya kufundishwa na makocha wanne tofauti msimu huu imezua maswali, lakini kilichosemwa na viongozi wa klabu hiyo akiwemo Ofisa Habari, Ally Kamwe ni kwamba mabadiliko hayo yamefanyika mapema ili kuendana na uhalisia ulivyo kwani wanapoona timu haichezi vizuri, wanachukua hatua za haraka kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.
Kauli hiyo inaonesha namna gani makocha hao walioingia na kutoka ndani ya Yanga na Simba kuwa bado hajawatoa kile kinachohitajika na kufanya mashabiki na hata viongozi kuteseka licha ya kwenye makaratasi wapo waliofanya vizuri lakini wakaondoshwa.
YANGA
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, walianza na Romain Folz kisha timu ikawa chini ya usimamizi wa muda wa Patrick Mabedi, akaja kocha mkuu Pedro Goncalves, alipoondolewa, Abdihamid Moalin amekabidhiwa kikosi akishirikiana na Mabedi.
Folz aliyetambulishwa Julai 2025, aliondoka muda mfupi baada ya Yanga kufungwa 1-0 katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers, Oktoba 18, 2025.
Folz aliyetambulishwa Julai 23, 2025 na kuondoka Oktoba 18, 2025, alidumu kwa takribani siku 86, akiiongoza kucheza mechi sita pekee za mashindano akishinda nne, sare moja sawa na aliyopoteza.
Folz alianza kwa ushindi wa 1-0 Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na kubeba ngao hiyo, kisha ushindi wa 3-0 katika hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Wiliete na marudiano akashinda 2-0 na kufuzu hatua inayofuata.
Katika ligi ni mechi mbili akishinda 3-0 dhidi ya Pamba Jiji, akaja kutoka 0-0 na Mbeya City, baada ya hapo akamaliza na kichapo cha 1-0 dhidi ya Silver Strikers ugenini katika mtoano kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, safari ikaishia hapo akiwa ameondoka ameacha Ngao ya Jamii katika kabati la Yanga.
Patrick Mabedi akapewa kazi ya kuiongoza Yanga mechi ya marudiano dhidi ya Silver Strikers na kupata ushindi wa mabao 2-0, akaivusha timu kwenda makundi kwa jumla ya mabao 2-1.
Ndipo akatua Pedro ambaye amesimamia mechi 35 za mashindano tofauti akishinda Kombe la Mapinduzi 2026 kwa rekodi ya kushinda mechi zote nne ikiwemo kuzifunga Singida Black Stars hatua ya nusu fainali na Azam katika fainali.
Kwa ujumla, Pedro ameondoka Yanga baada ya siku 172 kutoka Oktoba 25, 2025 hadi Mei 6, 2026 akiiongoza timu hiyo kucheza mechi 35 za mashindano matano tofauti na kushinda kombe moja, huku pia akipoteza fainali moja.
Rekodi zake zinaonesha Ligi Kuu Bara amesimia mechi 19 akishinda 14 na sare nne, hajapoteza. Ligi ya Mabingwa Afrika mechi sita akishinda mbili sawa na sare na alizopoteza, huku Kombe la FA ikiwa ni mechi tatu alizoshinda zote.
Ukija Kombe la Mapinduzi ni mechi nne alizoshinda zote hadi kubeba kombe, huku Kombe la Muungano alilopoteza fainali mbele ya Simba, akishinda mechi mbili kati ya tatu.
Katika siku 172, Pedro ameshuhudia kikosi chake cha Yanga kikifunga mabao 68 yaliyotokana na ushindi wa mechi 25, sare saba na kupoteza tatu, sambamba na kuruhusu mabao 12, akiacha kombe moja kabatini.
SIMBA
Hii ndiyo timu ambayo imeongoza kwa benchi lake la ufundi kusimamiwa na idadi kubwa ya makocha msimu huu kulinganisha na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu.
Ilianza na Fadlu Davids ambaye aliondoka kabla Ligi Kuu haijaanza lakini aliiongoza timu hiyo katika mashindano ya Ngao ya Jamii ya kufungua msimu akipoteza mbele ya Yanga, kisha mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali ugenini dhidi ya Gaborone United aliyoshinda 1-0.
Baada ya Fadlu kuondoka, Simba ilimchukua kwa muda Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye ilimpa jukumu la kuiongoza katika mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana ya marudiano iliyomalizika kwa sare ya 1-1 na timu hiyo kufuzu hatua ya pili.
Kibarua cha Morocco kilipokamilika, Simba ikawa chini ya Selemani Matola katika mechi za Ligi Kuu Bara akishinda zote mbili dhidi ya Fountain Gate (3-0) na Namungo (3-0).
Baadaye ikamuajiri Dimitar Pantev aliyetambulishwa Oktoba 3, 2025, akadumu kwa siku 61 akiondoka Desemba 2, 2025.
Pantev aliyetua Simba akitokea Gaborone United ya Botswana sambamba na msaidizi wake, Boyko Simeonev, aliiongoza timu hiyo kucheza mechi tano za mashindano tofauti, akishinda mbili, sare moja na kupoteza mbili.
Ilielezwa kwamba, matokeo yasiyoridhisha ndiyo yamechangia Pantev kusitishwa mkataba wake kwani Simba ilipoteza mechi zote mbili za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikianza kufungwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Petro Atletico, kisha ikachapwa ugenini mabao 2-1 na Stade Malien.
Katika Ligi ya Mabingwa, pia Simba chini ya Pantev ilishinda mechi moja ugenini dhidi ya Nsingizini Hotspurs kwa mabao 3-0 ikiwa ni hatua ya pili kuwania kufuzu makundi. Pia aliiongoza kushinda 2-1 ugenini ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania.
Matola akashika tena usukani akishinda 3-0 dhidi ya Mbeya City, kisha kichapo cha 2-0 kutoka kwa Azam, zote zikiwa mechi za Ligi Kuu Bara.
Desemba 19, 2025, Simba ikamchukua Steve Barker aliyepo hadi sasa akiwa tayari ameshinda Kombe la Muungano kwa kuichapa Yanga.
Barker anaonekana kuwa na mwendo mzuri ambapo ukiweka kando ubingwa wa Muungano, pia amepoteza mechi moja ya nusu fainali Kombe la Mapinduzi 2026 mbele ya Azam.
Lakini kwenye ligi hajapoteza akishinda kumi na sare saba.
Upande wa Kombe la Mapinduzi, alishinda mbili na kupoteza moja kati ya mechi tatu, huku Kombe la Muungano akishinda zote tatu sawa na zile za Kombe la FA ambapo Simba ipo robo fainali.
WASIKIE WADAU
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Yanga , Pan Africans, Peter Tino, amesema nyakati hizi kila mtu anajua mpira wa miguu, jambo lililomuwia ugumu kuchambua kwa nini klabu hizo zinafukuza makocha.
“Jambo la msingi ni kila mtu asimamie wajibu wake kikamilifu, ili lawama zinapokuja ziwe ni zile ambazo mtu anastahili,” amesema Tino.
Staa mwingine wa zamani wa Yanga, Nonda Shaban amesema timu haiishi katika pitch (sehemu ya kuchezea), yapo mambo mengi nje ya uwanja, hivyo uamuzi unapotoka unaweza kushangaza ingawa huenda ukawa wenye manufaa.
“Mfano kuna makocha ambao hawashauriwi, hapo inakuwa ngumu kwa viongozi kuendelea naye, aliyeondoka licha ya timu kutokupoteza mechi ila ilikuwa inacheza chini ya kiwango ni vile ilikutana na timu ambazo hazikuwa na chelenji nzuri za kuifunga Yanga,” amesema Shaban na kuongeza;
“Yanga kabla ilikuwa na makocha wenye viwango vya juu kama Miguel Gamondi, Nasreddine Nabi mashabiki walizoea kuona timu ikifanya vizuri, sasa alipokuja Pedro hawaoni hilo, pia alishindwa kuwaunganisha wachezaji na kuwatumia vizuri, mfano sabu ya kumchezesha Maxi Nzengeli namba mbili wakati Kibwana Shomari yupo nje mechi dhidi ya KMC, unajiuliza ni chuki ama kitu gani, ila waliyoko ndani ndiyo wanajua ukweli.
“Kwa upande wa Simba wana falsafa yao ndiyo maana unaona makocha wanakuja na kuondoka lakini bado msaidizi anasalia ni yule yule, Seleman Matola.”
Staa mwingine wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Steven Mapunda ‘Garincha’ amesema:
“Kila kocha anakuwa na mifumo yake pia kuna wakati mwingine makocha wanahitaji kupewa muda pamoja na wachezaji, lakini sasa timu za Simba na Yanga zina presha muda wote, zinazoweza kusababisha timu kukosa utulivu kwa muda mrefu.”