DKT KIJAJI: AFCON 2027 si mpira tu, ni utalii
Muktasari:
- Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba kati ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na uzinduzi wa ofisi za uratibu wa AFCON 2027, Kijaji alisema ushirikiano huo ni matokeo ya uzalendo na kujitoa katika kuhakikisha maandalizi ya mashindano hayo yanafanikiwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, DKT Ashantu Kijaji, amesema Fainali za Mataifa ya Afrika AFCON 2027 si mashindano ya soka pekee, bali ni fursa kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa, kukuza utalii, kuongeza mapato na kufungua milango ya uwekezaji kupitia ujio wa wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba kati ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na uzinduzi wa ofisi za uratibu wa AFCON 2027, Kijaji alisema ushirikiano huo ni matokeo ya uzalendo na kujitoa katika kuhakikisha maandalizi ya mashindano hayo yanafanikiwa.
Alisema mashindano hayo yanatarajiwa kuleta fursa nyingi za kiuchumi kutokana na ujio wa timu, mashabiki, watalii, wawekezaji na wageni wengine, ambao wataongeza mahitaji ya huduma za malazi, usafiri, migahawa na maeneo ya burudani, hivyo kunufaisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii.
"AFCON si soka pekee, bali inawakutanisha mamilioni ya watu na kutoa fursa za kiuchumi. Ushirikiano huu unatoa nafasi ya kuitangaza nchi yetu," alisema Kijaji.
Aliongeza kuwa wizara hiyo inaitazama AFCON 2027 kama kichocheo cha kuitangaza Tanzania kupitia vivutio vyake vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Zanzibar na Kisiwa cha Mafia, pamoja na vivutio vya wanyamapori vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.
Kijaji alisema maandalizi ya Tanzania hayaishii kwenye viwanja vya michezo, bali pia yanahusisha kuhakikisha hoteli za madaraja yote zinakuwa tayari kupokea wageni, kuimarisha huduma za utalii na kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili wageni watakaokuja kutazama mpira wapate nafasi ya kutembelea vivutio vya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisisitiza kuwa AFCON 2027 inapaswa kuangaliwa kama uwekezaji wa kimkakati wenye manufaa ya muda mrefu badala ya tukio la wiki chache, huku Tanzania ikishirikiana na wenyeji wenzake Kenya na Uganda kuhakikisha Afrika inaona utayari wa ukanda wa Afrika Mashariki kuandaa mashindano hayo kwa mafanikio.