Teknolojia ya mstari yazua utata
Muktasari:
- Porto ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza ndani ya dakika mbili, baada ya Oussama Targhalline kujifunga mwenyewe akijaribu kuzuia mpira wa chini uliopigwa na Oskar Pietuszewski.
LISBON, Ureno: TEKNOLOJIA ya kubaini kama mpira umevuka mstari wa goli (Goal-line Technology) karibu iinyime Porto ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Feyenoord katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kutoa taarifa isiyo sahihi kuwa wenyeji hao walikuwa wamesawazisha dakika za mwisho.
Porto ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza ndani ya dakika mbili, baada ya Oussama Targhalline kujifunga mwenyewe akijaribu kuzuia mpira wa chini uliopigwa na Oskar Pietuszewski.
Hata hivyo, Feyenoord ilidhani imefanikiwa kusawazisha dakika ya 88, wakati mwamuzi Irfan Peljto alipoashiria kuwa kichwa cha Nacho Ferri kilikuwa kimevuka mstari wa goli la Porto.
Awali, Peljto hakuzingatia malalamiko ya wachezaji wa Porto na badala yake alielekeza kidole kwenye saa yake, kifaa kinachowapa waamuzi taarifa kuhusu kama mpira umevuka mstari wa goli kikamilifu.
Hata hivyo, mwamuzi msaidizi wa video (VAR) aliingilia kati muda mfupi baadaye na bao hilo likakataliwa baada ya marudio ya picha kuonyesha kuwa mpira uliopigwa kwa kichwa na Ferri haukuwa umevuka mstari wa goli ulipogonga mwamba wa kulia. Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Porto katika michuano ya Ulaya, baada ya kuanza vibaya kwa kupoteza mechi zake tatu za kwanza.
Kwa upande wa Feyenoord, matokeo hayo yameendeleza mwenendo mbaya wa timu hiyo, ambayo haijashinda katika mechi saba zilizopita kwenye mashindano yote, hali inayoiweka katika hatari kubwa ya kushindwa kufuzu hatua ya mtoano.
Feyenoord itasafiri kwenda Norway kuvaana na Viking Desemba 8, huku Porto ikitarajiwa kwenda Anfield kucheza dhidi ya Liverpool siku inayofuata.