Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yafanya kufuru ulaya

Muktasari:

MO ameamua kutumia fedha za maana kabisa kuifanya Simba kuwa timu tishio Afrika na hilo linadhihirika kwa yale yanayoendelea hapa Uturuki, ambako Simba imeweka kambi ikijifua kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataif

BILIONEA wa Simba, Mohamed Dewji (MO) amepania na kamwe hataki utani katika kuhakikisha Wekundu wa Msimbazi wanarejesha heshima ya soka la Tanzania kimataifa.

MO ameamua kutumia fedha za maana kabisa kuifanya Simba kuwa timu tishio Afrika na hilo linadhihirika kwa yale yanayoendelea hapa Uturuki, ambako Simba imeweka kambi ikijifua kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Simba imeweka kambi katika Hoteli ya The Green Park iliyopo kwenye Mji wa Kartepe, ambako kuna maajabu ya kila aina na kuwafanya wachezaji kukutana na mambo tofauti na yale waliyoyazoea. The Green Park hutembelewa na idadi kubwa ya wageni kila siku, ambao huweka kambi asubuhi na jioni huondoka kurejea kwenye miji mingine.

Lakini kwanza achana na hilo la maajabu yanayozunguka kambi hiyo, ishu kubwa ni gharama ambazo MO ametumia kuiweka klabu hiyo kambini na maisha yake kwa jumla.

Hapa Mwanaspoti ambalo limeweka kambi huku Uturuki linakueleza japo kwa uchache tu mambo yalivyo na gharama ambazo Simba imetumia kufanikisha kambi yake.

HOTELI

Kwa kawaida tu, kama umefika eneo la The Green Park ukiwa na stresi zako basi hali ya hewa na mandhari iliyopo, unasahau kila kitu na kujiona mtu tofauti kabisa. Wakati Simba inatafuta mahali kwa kuweka kambi, ilionyeshwa hoteli kadhaa lakini, walipofika hapa wakasema imetosha.

Gharama ya kuweka kambi kwenye hoteli hii ambayo ina huduma zote muhimu ikiwemo viwanja vya soka, tenisi, gofu, mabwawa ya kuogelea, vyumba vya kutosha na misosi ya kila aina sio za kitoto hata kidogo.

Lakini gharama zake hubadilika kulingana na majira, ambapo wakati wa baridi gharama hupanda maradufu kutokana na kuwa na wageni wengi kutoka pande mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa wafanyakazi wa hoteli hii, gharama za vyumba wakati wa majira ya joto ni kati ya Dola 85 (zaidi ya Sh150,000) na Dola 200 (zaidi ya Sh 400,000) kwa vyumba vya kawaida. Lakini, vile vya kishua gharama ni kati ya Dola 300 hadi 500 na wakati wa majira ya baridi ambapo, wageni wengi hutembelea hapo gharama inafika Dola 5,000 (zaidi ya Sh 10 milioni). Kibongobongo Sh10 milioni unanunua kiwanja chako kizuri kabisa na kuanza kufyatua matofali maeneo ya Mbagala, Kigamboni na hata Chanika, Dar.

Kama ulikuwa umezoea kuona michezo ya kucheza kwenye barafu kwenye runinga, basi mastaa wa Simba wamejionea kwa macho na wengine kuamua kushiriki kabisa.

Kwa Simba wanalipa chumba kimoja Dola 120 (265,000) kwa siku kwa kila mchezaji ikiwa ni pamoja na gharama za chakula, usafiri na matumizi ya vifaa vingine kama viwanja vya michezo.

Kikosi cha Simba kina wachezaji 27, benchi la ufundi wanane na viongozi wawili. Katika hoteli hii Simba imegharamia vyumba 24 ambapo, wachezaji wanatumia vyumba 14 na vilivyobaki ni kwa ajili ya benchi la ufundi na viongozi. Kwa maana hiyo, Simba imelipia Dola 40,320 (Sh. 92 milioni) kwa wiki mbili ambazo wamepiga kambi hapa Uturuki.

Sifa ya ziada ni kwamba, hoteli hii ni kubwa na ina uwezo wa kuchukua na kuzihudumia bila shida timu zaidi ya 30 kwa wakati mmoja.

Pia, ina majengo na viwanja ambavyo ni maalumu kwa ajili ya timu za soka na mpira wa kikapu kuweka kambi.

Kwa sasa Simba ni miongoni mwa timu 14 ikiungana na nyingine kutoka Algeria, Misri, Tunisia, Morocco na Mali, Asia nchi za Saudi Arabia, Oman, Dubai, China na nchi za Ulaya kama wenyeji Uturuki, Uswisi na Italia, ambazo ziko hapa zikiendelea kujifua.

Hoteli ina vyumba vya kawaida vya kitanda kimoja (single) na watu wawili (double), ambavyo jumla yake ni 250. Pia, kuna apartimenti ambazo kila moja ina vyumba viwili vyenye vitanda viwili na sebule.

MISOSI YAKE SASA

Hapa kwenye misosi hakuna kinachokosekana na mastaa wa Simba wanajiachia kwelikweli. Yale mambo ya kushangaa mastaa wakubwa wa Ulaya wakipiga kuku mzima na mbogamboga kibao, hapa mbona yapo na ni kawaida sana. Msosi wa Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Adam Salamba na wengine kibao mbona ukiona unaweza kukimbia mwenyewe.

Kwenye menyu ya Simba kinachokosekana ni ugali, lakini mazagazaga mengine yapo tena ya kimwaga si unajua mambo ya bufee.

Panga pangua msosi wa wachezaji wa Simba huwezi kukosa samaki, wali, tambi, ndizi, viazi, mikate, chapati, kuku, nyama na mboga za majani za kutosha ndio mpango mzima.

UWANJA WA MAZOEZI

Hoteli hii ina viwanja vya kisasa vya michezo vyenye vifaa vyote muhimu kwa timu katika mazoezi, viwanja vya kutosha ambapo vya soka ni saba, kati ya hivyo vitano vikubwa na viwili vidogo, pia uwanja mmoja wa mchezo wa mpira wa kikapu.

Kuna mabwawa ya kuogelea ndani ya hoteli ambayo hutumiwa na wachezaji mbali na ya nje, kuna sauna na gym ya mazoezi. Matumizi ya gharama za vifaa hivi yamejumuishwa kwenye malipo ya malazi.

USAFIRI UWANJANI

Kambi ya Simba hapa Uturuki ipo umbali wa kilometa 164 kutoka jijini Istanbul, ambapo kwa mwendo wa gari ni wastani wa masaa matatu. Mara baada ya kutua hapa, kikosi cha Simba kilisafiri kwa basi maalumu la hoteli hiyo, ambapo gharama yake ni Dola za Marekani 500 sawa na Sh1.2milioni. Huku msafara wa viongozi ukisafarishwa kutoka Uwanja wa Ndege kuja kambini kwa 600 sawa na Sh14 milioni. Pia, kuna gharama nyingine za dola 300 (Sh685,510) kwa ajili ya usafiri wa wachezaji kwenda kutalii na kufanya shopingi.

Lakini achana na usafiri wa ndani ambao sio ishu kubwa kabisa, MO na Simba yake wamemwaga mamilioni ya shilingi pia kwenye usafiri wa mwewe kutoka Dar es Salaam kuja Uturuki, ambapo tiketi ya kwenda na kurudi kwa kila mchezaji ni Dola 1,800 ambapo kwa msafara mzima ni Dola 66,600 sawa na Sh151.9 milioni.

Kwa data ambazo Mwanaspoti imezikusanya ni kuwa Simba imetumia Sh 250 milioni kwa kambi hiyo. Hata hivyo, hapa hujaweka zagazaga mengine ambayo Mwanaspoti limechemka kupata data zake kutokana na wahusika kufanya siri kubwa ikiwemo posho za makocha, viongozi na wachezaji kwa muda wote waliokuwa kambini hapa Uturuki.

Pia, kuna gharama nyingine za vibali vya kuingia hapa Uturuki ambapo kwa mtu mmoja hulipa kati ya Dola 60 hadi 100, ambapo kwa msafara nzima sio pesa ya kitoto. Vilevile kuna gharama ambazo zimekuwa zikifanyika bila kuwekwa bayana, hivyo kwa haraka haraka Simba inaweza kuwa imetumia zaidi ya Sh 500 milioni hadi kukamilisha kambi hiyo, ambayo imewapa makali kinoma.

MAAJABU YENYEWE

Simba imetua kuweka kambi hapa wakati wa majira ya joto, lakini hali ya hewa ya hapa imekuwa ikiwashangaza wengi kutokana na namna inavyobadilika kila wakati.

Iko hivi, unaweza kuona jua kali linawaka, baada ya hapo likaja wingu zito na kufunika eneo lote kiasi ambacho hakuna mtu anayeweza kumwona mwenzake. Wingu hilo linaweza kudumu kwa kwa dakika tano mpaka 10 kisha linapotea kabisa.

Pia, unaweza kuona jua linawaka, muda huo huo ikaja mvua kubwa ambayo pia hainyeshi muda mrefu ni dakika mbili mpaka 10, kisha inakata na jua linawaka.

Mvua yenyewe, inaweza kunyesha kubwa upande mmoja wa hoteli na mwingine ukawa mkavu kabisa. Hali hiyo imekuwa ikibadilika kila dakika kwa siku na mambo yanaendelea.

SIMBA MZUKA MWINGI

Mbali na hali ya hewa kuwa nzuri, wachezaji wa Simba, Kocha Patrick Aussems na benchi lake la ufundi wanapata mzuka mwingi kutokana na mazingira.

Ni mahali tulivu kwani hoteli ipo juu ya mlima na imejitenga peke yake. Mji wenye makazi ya watu uko chini ya mlima kutoa The Green Park mpaka mjini Kartepe kwa gari ni mwendo wa dakika 20.

Hakuna vurugu licha ya timu kuwa nyingi sehemu moja, kila moja ina mipango yake na Aussems anasema: “Hii ndiyo kambi inayohitajika, hapa tunapata kila kitu kama vifaa vya michezo, mazoezi ya utulivu, mechi za kirafiki, chakula na kila kitu. Uwepo wa timu nyingi hotelini hapo umempa urahisi kocha Aussems kupata timu bora za kukipima kikosi chake.

Kuna vifaa vyote muhimu kwa timu katika mazoezi, viwanja vya kutosha ambapo vya soka ni saba, kati ya hivyo vitano vikubwa na viwili vidogo, pia uwanja mmoja wa mchezo wa mpira wa kikapu.

Kuna mabwawa ya kuogelea ndani ya hoteli ambayo hutumiwa na wachezaji mbali na ya nje, kuna sauna na gym ya mazoezi.

Hali ya hewa, ndani wameweka viyoyozi vya joto na baridi ,hivyo haiwezi kuathiri mtu.