Shalulile, Toure waing'arisha Yanga, Kagera Sugar ikiendeleza uteja
Muktasari:
- Katika mechi hiyo, mshambuliaji Peter Shalulile alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 26, akitumia vyema pasi ya Maxi Nzengeli likiwa ni la sita kwake kwenye ligi msimu huu.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wameendelea kukusanya pointi tatu baada ya leo kuifunga Kagera Sugar mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji Peter Shalulile alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 26, akitumia vyema pasi ya Maxi Nzengeli likiwa ni la sita kwake kwenye ligi msimu huu.
Wakati Kagera Sugar inayofundishwa na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze ikipambana kwa lengo la kusawazisha, ilishtukizwa kwa kufungwa bao la pili dakika ya 32, lililofungwa na beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Zimbwe JR', akimalizia pasi ya Stephane Aziz KI.
Mabao hayo mawili yakaipeleka Yanga hadi dakika 45, za kipindi cha kwanza kifua mbele, ikiwa ni mwendelezo mzuri kwa timu hiyo, tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho raia wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi aliyeondoka Oktoba 24, 2026, baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba wake.
Kipindi cha pili, Kagera Sugar iliingia Kwa mkakati mzuri wa kutengeneza mashambulizi ya kusawazisha mabao hayo, japo, uimara wa Yanga katika kuzuia uliifanya kushindwa kutekeleza mpango huo vizuri na kupoteza mechi.
Kwa upande wa Yanga, iliendelea pia kutengeneza mashambulizi makali na jitihada hizo zilizaa matunda dakika ya 88, baada ya Cheikh Ibrahima Toure kuifungia la tatu kwa kichwa akimalizia pasi ya Mohamed Hussein 'Zimbwe JR'.
Wakati Kagera ikiamini mechi hiyo Imeisha kwa kupoteza mabao 3-0, ikajikuta ikifungwa bao la nne na Cheikh Ibrahima Toure dakika ya 90, akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Clement Mzize na kuwazidi ujanja mabeki wa kikosi hicho cha 'Wanankurukumbi'.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara tangu alipoondoka Manqoba, baada ya mechi iliyopita kushinda mabao 2-1, dhidi ya maafande wa Mashujaa FC, Oktoba 27, 2026, ikiwa chini ya kaimu kocha mkuu kwa sasa, Simo Dladla.
Katika mechi 10, iliyocheza Yanga hadi sasa, imeshinda minane, sare moja na kupoteza pia moja, ikiwa nafasi ya pili na pointi 25, nyuma ya watani zao wa jadi Simba inayoongoza na pointi 27.
Kwa upande wa Kagera iliyocheza 11, imeendeleza mwenendo mbaya hadi sasa, baada ya kushinda mechi moja tu, sare tatu na kupoteza saba, ikiwa mkiani mwa msimamo mwa nafasi ya 16, kufutia kukusanya pointi zake sita.
Kichapo cha leo, kimeifanya Kagera Sugar kuendeleza rekodi mbovu dhidi ya Yanga, kwani katika mechi zake 12, za Ligi Kuu Bara zilizopita, haijashinda yoyote, baada ya kuchapwa 10, kati ya hiyo na kutoa sare miwili, huku mara ya mwisho zilipokutana ilichapwa pia mabao 4-0, mechi iliyopigwa Februari 1, 2025.
Katika mechi hiyo ya Februari 1, 2025, mabao ya Yanga yalifungwa na Clement Mzize dakika ya 32, Mudathir Yahya dakika ya 60, Pacome Zouzoua kwa penalti ya dakika ya 78 na aliyekuwa pia mshambuliaji wa timu hiyo, Kennedy Musonda dakika ya 86.
Mara ya mwisho kwa Kagera Sugar kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara, ilikuwa ni ushindi wa mabao 3-0, Januari 15, 2020, kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam, ambapo wakati huo ilikuwa ikifundishwa na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Luc Eymael.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Eymael tangu ajiunge na Yanga, ambapo mabao ya Kagera yalifungwa na Yusuph Mhilu, Ally Ramadhan 'Kagawa' na Peter Mwalyanzi, huku aliyekuwa kiungo wa Yanga, Mohamed Issa 'Banka' akionyeshwa kadi nyekundu.
Kwa maana hiyo, tangu Januari 15, 2020, hadi sasa, Kagera Sugar haijawahi kuifunga Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara, ikitimiza miaka sita, ikiwa ni mwenendo mbaya kwa kikosi hicho cha 'Wanankurukumbi'.