Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi yacheka dakika za jioni, Geita ikilala Ushirika

POLISI Pict (1)

Muktasari:

  • Ushindi huo kwa Polisi uliokuja kufuatia bao la kujifunga la beki Twalib Muhenga dakika ya 90+3, umewafanya wenyeji kufikisha pointi 15 na kupanda hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, matokeo yaliyorejesha tabasamu kwa mashabiki wake baada ya kipindi cha kusubiri ushindi.

Dakika za mwisho za ngongeza zimekuwa mwokozi wa Polisi Tanzania baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo Novemba 1, 2026 kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ushindi huo kwa Polisi uliokuja kufuatia bao la kujifunga la beki Twalib Muhenga dakika ya 90+3, umewafanya wenyeji kufikisha pointi 15 na kupanda hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, matokeo yaliyorejesha tabasamu kwa mashabiki wake baada ya kipindi cha kusubiri ushindi.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, ulionekana kuelekea kumalizika kwa sare, lakini Geita Gold ilijikuta ikivuna machungu wakati Muhenga akitaka kuuokoa mpira uliokuwa ukielekezwa langoni mwao akajikuta akiusindikiza moja kwa moja nyavuni.

Bao hilo lilitokana na mpira mrefu uliopigwa na beki wa Polisi Tanzania, Denis Mushi karibu na katikati ya uwanja ambao ulizua mkanganyiko katika safu ya ulinzi ya Geita Gold na kuifanya timu hiyo kulipa gharama dakika ambazo hazikuwa na nafasi tena ya kurekebisha matokeo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila, amesema kikosi chake kimeumia kupoteza pointi zote tatu, hasa kwa kuwa bao lilipatikana wakati mchezo ukielekea ukingoni.

"Tumeweza kupoteza mchezo kwa maana wenzetu wamepata bao katika dakika ambazo hazikuwa za kutarajia. Ni dakika za nyongeza, mpira ulikuwa unaenda ukingoni. Wamepiga long ball, tumeweza kuucheza na kumchanganya kipa na kupata bao," amesema Katwila.

Amesema licha ya kupoteza mchezo huo, kikosi chake kitaitumia kipindi cha mapumziko kufanya marekebisho kabla ya ligi kurejea, akilenga kuimarisha timu ili iweze kurejea ikiwa na nguvu mpya.

Kwa upande wa Polisi Tanzania, mwakilishi wa benchi la ufundi amesema ushindi huo umetokana na uvumilivu wa wachezaji waliopambana hadi dakika za mwisho, licha ya changamoto ya uchovu.

Amesema maandalizi ya mchezo huo hayakuwa rahisi kutokana na muda mfupi wa maandalizi, baada ya kikosi kusafiri Oktoba 29 na kufika Oktoba 31, huku kikiwa na muda mchache wa kufanya mazoezi na kuelekezwa mbinu za mchezo.

"Niwapongeze vijana wangu, wameweza kusikiliza maelekezo, wamecheza na kupambana mpaka dakika ya mwisho. Tumeweza kupata ushindi," amesema.

Ameongeza kuwa sasa wanajiandaa na michezo inayofuata, ikiwamo dhidi ya Yanga inayotarajiwa kuchezwa Novemba 20, 2026, huku benchi la ufundi likipanga kutumia kipindi cha mapumziko kuandaa kikosi.

Matokeo hayo yamewaacha mashabiki wa Geita Gold wakiwa na masikitiko, lakini wakionyesha matumaini ya kuona timu yao ikirejea kwa nguvu katika michezo ijayo.

Shabiki wa timu hiyo, Ndakama Ndakama, ambaye pia ni Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, amesema timu yao ilitengeneza nafasi za kufunga, lakini ilishindwa kuzitumia na hatimaye kuadhibiwa kwa kosa moja la dakika za mwisho.

"Matokeo ni sehemu ya mchezo. Kuna kufungwa, kutoka sare na kushinda. Haijawa bahati kwetu, tumetengeneza nafasi lakini hatujaweza kuzitumia. Mwisho tumefanya kosa na kujifunga, hakuna namna, tunarudi," amesema.

Amesema anaamini benchi la ufundi limeyaona mapungufu yaliyojitokeza na litayafanyia kazi wakati wa mazoezi ili timu irejee ikiwa imara zaidi.

Naye Augustino James Peter, amesema wamepokea matokeo hayo kwa masikitiko kwa kuwa walifika Moshi wakiwa na matumaini ya kuondoka na ushindi.

Amesema bao walilofungwa limeonyesha upungufu unaohitaji kurekebishwa, huku akieleza imani yake kwa benchi la ufundi kufanya kazi ya kurejesha makali ya timu hiyo.

Kwa upande wa mashabiki wa Polisi Tanzania, Fredrick Mchafu, amesema ushindi huo umewapa furaha kubwa kutokana na muda ambao wamekuwa wakisubiri timu yao ipate matokeo mazuri.

"Ushindi wa leo umetufurahisha sana sisi mashabiki wa Polisi Tanzania baada ya timu yetu kukaa muda mrefu bila kupata ushindi. Leo tumepata ushindi, japokuwa ilikuwa dakika za jioni, lakini ndiyo maana ya dakika 90. Mpira hauishi mpaka dakika 90 ziishe," amesema.

Mchafu amesema anaamini mchezo dhidi ya Yanga utakuwa mgumu, lakini Polisi Tanzania ina nafasi ya kufanya vizuri ikiwa itaendeleza kiwango na morali iliyoonyeshwa dhidi ya Geita Gold.

Amesema hata Yanga imekuwa ikipitia matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya michezo ya hivi karibuni, jambo linalompa matumaini kuwa Polisi Tanzania inaweza kupambana na kupata matokeo mazuri.