Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Safu ya ulinzi Coastal tatizo

Muktasari:

  • Timu hiyo ya Tanga imekuwa na wakati mgumu wa kujilinda, ikiruhusu mabao matano zaidi ya iliyofunga, hali inayodhihirisha changamoto iliyopo katika safu hiyo na kumlazimu Fikiri kuweka mkazo katika kuiboresha kabla ya michezo inayofuata.

SAFU ya ulinzi imeendelea kuwa tatizo kwa Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias, baada ya kukiri kuwa eneo hilo linahitaji marekebisho makubwa kufuatia kuruhusu mabao 16 katika mechi 12 za Ligi Kuu Bara msimu huu.

Timu hiyo ya Tanga imekuwa na wakati mgumu wa kujilinda, ikiruhusu mabao matano zaidi ya iliyofunga, hali inayodhihirisha changamoto iliyopo katika safu hiyo na kumlazimu Fikiri kuweka mkazo katika kuiboresha kabla ya michezo inayofuata.

Coastal Union imefunga mabao 11 na kuruhusu 16 katika mechi 12, huku ikishinda nne, sare mbili na kupoteza sita, matokeo yaliyoifanya kukusanya pointi 14 na kushika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi.

Kocha huyo alisema changamoto hiyo imeendelea kuwapa wakati mgumu, hasa baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Pamba Jiji kwa mabao 3-2, licha ya kikosi chake kuonyesha ushindani na kuwa na nafasi ya kupata matokeo mazuri.

Fikiri alisema kipigo hicho kimewaumiza kwa sababu maandalizi yao yalilenga kuondoka na pointi, lakini kushindwa kutumia vizuri nafasi walizopata na makosa yaliyojitokeza kuliwafanya washindwe kufikia lengo hilo.

“Matokeo ya mchezo dhidi ya Pamba yametuuma kwa sababu tulikuwa na matarajio ya kupata matokeo mazuri. Tulicheza mchezo mzuri na tulionyesha ushindani, lakini bahati mbaya hatukuweza kupata kile tulichokuwa tunakitafuta,” alisema.

Alisema pamoja na kuona baadhi ya mambo yakikwenda vizuri katika mchezo huo, bado kuna mapungufu yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuhakikisha makosa hayajirudii na kuendelea kuigharimu timu.

“Tunatambua kuna mambo tuliyafanya vizuri, lakini pia kuna maeneo ambayo hatukufanya vizuri. Hatuwezi kuridhika na namna tulivyopoteza mchezo kwa sababu tulikuwa na nafasi ya kupata matokeo,” alisema.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Geita Gold, Fikiri alisema eneo la ulinzi litakuwa miongoni mwa vipaumbele vyao katika mazoezi, akisisitiza umuhimu wa kurekebisha makosa yanayowapa wapinzani nafasi za kufunga.

“Kabla ya mchezo wetu unaofuata tuna kazi ya kufanya kwenye safu ya ulinzi. Tumekuwa tukikutana na changamoto katika eneo hilo na tunahitaji kurekebisha makosa yanayojitokeza,”.

Aliongeza kuwa wanahitaji kwenda Geita wakiwa wamejiandaa vizuri zaidi ili kuepuka kurudia makosa yaliyowagharimu katika michezo iliyopita.