Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AFCON 2027 itakavyoibeba Tanzania kiutalii

Muktasari:

  • Ushirikiano huo unaofanyika chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, unalenga kuhakikisha AFCON 2027 haibaki kuwa mashindano ya soka pekee, bali inakuwa jukwaa la kuitangaza Tanzania, kuvutia watalii na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia mamilioni ya watu watakaofuatilia michuano hiyo.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), zimeingia makubaliano ya ushirikiano yatakayoiwezesha Tanzania kutumia fursa ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kujitangaza kimataifa kupitia utalii, uwekezaji na vivutio vyake mbalimbali.

Ushirikiano huo unaofanyika chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, unalenga kuhakikisha AFCON 2027 haibaki kuwa mashindano ya soka pekee, bali inakuwa jukwaa la kuitangaza Tanzania, kuvutia watalii na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia mamilioni ya watu watakaofuatilia michuano hiyo.

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika sambamba na uzinduzi rasmi wa ofisi za uratibu za CAF za AFCON 2027 jijini Dar es Salaam, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, alisema AFCON ni zaidi ya mchezo wa soka kwa kuwa inatoa fursa kubwa ya kiuchumi kupitia ujio wa timu, mashabiki, watalii, wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Alisema wageni hao wataongeza mahitaji ya huduma za malazi, usafiri, migahawa na maeneo ya burudani, hali itakayochochea shughuli za kiuchumi na kunufaisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii.

“AFCON si soka pekee, bali inawakutanisha mamilioni ya watu na kutoa fursa za kiuchumi. Ushirikiano huu unatoa nafasi ya kuitangaza nchi yetu,” alisema Kijaji.

Aliongeza kuwa, Serikali inaitazama AFCON 2027 kama fursa ya kuitangaza Tanzania kupitia vivutio vyake mbalimbali ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Zanzibar na Kisiwa cha Mafia, pamoja na vivutio vya wanyamapori vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adamu, alisema amevutiwa na vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, akieleza kuwa mashindano hayo yatatoa nafasi kwa nchi hiyo kujitangaza zaidi katika ulimwengu wa soka na kuvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

“Ni furaha kubwa kwangu kuwepo leo hapa, najivunia kuona nchi iliyopiga hatua kubwa ya utalii ambayo ni moja ya sifa inayoendelea kuitangaza Tanzania nje ya mipaka ya nchi,” alisema.

Aidha, Adamu alisema hatua ya Kiswahili kuidhinishwa kuwa mojawapo ya lugha rasmi za CAF ni ishara ya mshikamano uliopo kati ya nchi tatu zitakazoandaa AFCON 2027, ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Ikumbukwe kuwa CAF ilifikia uamuzi wa kuidhinisha Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha rasmi za Shirikisho hilo katika Mkutano Mkuu wa 48 uliofanyika Abuja, Nigeria, Novemba 21, 2026.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya AFCON 2027, Leodger Tenga, alisema Tanzania iko tayari kuonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kufanikisha mashindano hayo yatakayofanyika Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027, yakishirikisha wenyeji watatu, Tanzania, Kenya na Uganda.

Tenga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), alisema maandalizi yanaendelea vizuri na nchi imejipanga kutumia nafasi hiyo kuonyesha uwezo wake wa kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa.

“Ni fahari na heshima kubwa kwetu kwa Tanzania kupata nafasi hii muhimu. Nikiri wazi tumejiandaa vizuri na tupo tayari kuonyesha kwa vitendo namna nchi yetu ilivyodhamiria kuleta mageuzi makubwa,” alisema Tenga.

Uzinduzi wa ofisi hizo za uratibu za AFCON 2027 jijini Dar es Salaam umefanyika baada ya shughuli za ofisi hizo kuhamishwa kutoka Nairobi, Kenya, hatua inayoongeza umuhimu wa Tanzania katika uratibu wa maandalizi ya mashindano hayo.