Safari ya Stars AFCON inaanza leo mwanangu!
Muktasari:
Ni kweli safari ni hatua. Ndivyo ninaweza kuanza kuelezea safari yetu ya zaidi ya Kilomita 4,000 kutoka Dar es Salaam hadi Maseru, Lesotho kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) baina ya wenyeji na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.
KAMA Taifa Stars itafanikiwa kupata ushindi leo Jumapili kwenye pambano lao dhidi ya wenyeji Lesotho, hiyo itakuwa faraja kubwa kwangu na Watanzania wengine waliofunga safari kwa basi kwenda kuisapoti ugenini.
Nasema itakuwa ni faraja kwangu kutokana na ugumu wa safari ya kuifanya timu hiyo kutawaliwa na matatizo mbalimbali njiani.
Ni kweli safari ni hatua. Ndivyo ninaweza kuanza kuelezea safari yetu ya zaidi ya Kilomita 4,000 kutoka Dar es Salaam hadi Maseru, Lesotho kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) baina ya wenyeji na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.
Sio jambo rahisi kwa mtu kusafiri umbali mrefu kama huo kwa njia ya basi, kuvuka nchi tatu tofauti zenye hali tofauti ya hewa, utamaduni, sheria na taratibu zisizofanana, maeneo makubwa pamoja na mazingira yasiyolingana na yale ya nyumbani Tanzania.
Hata hivyo hamu ya kujifunza na kujionea hayo ikichagizwa na nia ya kuisapoti Taifa Stars pamoja na kuhabarisha umma wa Watanzania, ilitushawishi kusafiri umbali mrefu ardhini ilimradi tuweze kutimiza lengo tulilojiwekea.
Pamoja na yote, safari hiyo ya kwenda Lesotho haikuwa rahisi na nyepesi kama ilivyotarajiwa kwani pamoja na vitu na mazingira ya kusisimua njiani tulivyojionea, tulikumbana na misukosuko ya hapa na pale ambayo hata hivyo inabakia kuwa kumbukumbu ya kipekee na kihistoria kwa wote tuliosafiri na basi kwenda Lesotho.
Mwanzo wa safari
Dalili za ugumu wa safari ndefu ya kwenda Lesotho zilianza kuonekana mapema siku moja kabla ya kuanza baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusogeza mbele muda wa safari hiyo kutoka Jumanne alfajiri hadi saa 3 ya usiku siku hiyo.
Katika hali ya kushangaza, badala ya saa 3 usiku, safari hiyo ilichelewa kuanza hadi saa 6 kasoro ambapo takribani abiria 48 miongoni mwao wakiwa ni maofisa wa TFF, waandishi wa habari na mashabiki wa kawaida tulianza kuelekea Maseru tukiwa kwenye basi linalotumiwa na timu ya taifa.
Tulipofika Morogoro, basi liliongeza abiria watatu na mwingine mmoja alipandia Iringa.
Nuksi yaanzia Tunduma
Msafara ulipofika Tunduma tulilazimika kusimama kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kiuhamiaji kwa kugongewa mihuri kwenye hati zetu za kusafiria ili tuweze kuvuka kisheria nchi ya Zambia.
Baada ya kukamilisha taratibu za ugongaji mihuri hati za kusafiria, huku tukiamini kuwa tungeondoka mapema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, tulijikuta tukilazimika kuchelewa baada ya maofisa wa uhamiaji kulizuia basi letu kuingia Zambia kwa madai namba na cheti cha gari vilikuwa tofauti.
Tulilazimika kukaa hapo mpakani Tunduma kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 2 usiku tukisubiria turuhusiwe kutoka mahali hapo.
Vizuizi Zambia kilio
Kama kuna eneo ambalo lilifanya safari ichelewe ni kwenye nchi ya Zambia kutokana na vizuizi vya mara kwa mara ambavyo msafara ulikuwa umekutana navyo barabarani usiku huo wa manane ndani ya nchi hiyo.
Sheria ya Zambia hairuhusu magari kutembea usiku hivyo ililazimika kutumika nguvu na kazi ya ziada kuleta ushawishi kwa wahusika waruhusu tuendelee na safari.
Katika hali ya kushangaza katika vizuizi hivyo vya barabarani, askari walikuwa wanaomba rushwa ya fedha na pindi walipoona ugumu wa kupatiwa fedha hizo, walilazimisha msafara wetu ukae kwa muda mrefu eneo husika ili mradi tu waucheleweshe.
Katika vizuizi vitano ambavyo tulikutana navyo Zambia, kile kilichowekwa eneo la Kisoka ndicho kilituchelewesha zaidi kwa sababu tulisimama hapo kwa zaidi ya masaa mawili na nusu.
Mikosi ya njiani
Changamoto ya vizuizi ilikuwa ni kama mwendelezo wa majanga ambayo safari yetu ilikutana nayo njiani kwani baada ya hapo, mmoja wa wasafiri, Mshamu Mohammed ambaye ni mwandishi wa habari aliugua ghafla tumbo na kulazimika kupelekwa hospitali kutibiwa.
Mshamu alianza kusumbuliwa na tumbo akiwa njiani kutokana na kile kilichodaiwa kula chakula chenye sumu na baada ya maumivu ya usiku kucha, asubuhi na mapema aliwahishwa kwenye Hospitali ya 'Our Lady's Hospital' iliyopo wilaya ya Chilonga, Zambia na kutundikiwa dripu hadi alipopata nafuu.
Ukiondoa tatizo hilo la kuugua, mashabiki wengine wawili walipatwa na majanga ya kupoteza hati za kusafiria njiani ambapo mmoja aliipoteza katika mpaka wa Tunduma huku mwingine akiipoteza ndani ya basi.
Hilo lilipelekea mmoja ashushwe katika wilaya ya Kapiri Mposhi kuingojea hati yake ya kusafiria aliyoiangusha Tunduma, lakini mwingine alikwama kwenye mpaka wa kuingilia Zimbabwe na kulazimika kurudishwa nyumbani.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza, hati hizo zote za kusafiria zilipatikana baadaye.
Misukosuko iliendelea baada ya msafara kupotea njiani mara mbili ambapo moja ilikuwa ni katika njia ya kuelekea kwenye mpaka wa Zimbabwe na Afrika Kusini uitwao Beitbridge, lakini hata tulipoingia Afrika Kusini tulipotea njia wakati tunatoka Pretoria kwenda Johannesburg.
Vituko njiani
Safari yenye kundi kubwa la watu tofauti huwa haiwezi kukosa vituko, vimbwanga na vitimbi ambavyo huacha kumbukumbu pekee kwa walio kwenye msafara.
Miongoni mwa hivyo ni kitendo cha wadau waliokuwa kwenye msafara huo, kuchanga fedha na kununua mchele njiani eneo la Chimala Mbeya na baadaye kununua nyama na viungo vingine kwa ajili ya kupika pindi wakiwa njiani.
Mara kwa mara walikuwa wanataka kupika vyakula hivyo njiani lakini kutokana na umbali wa safari yenyewe, walishindwa kufanya hivyo.
Afrika Kusini kivutio
Msafara ulipoingia Afrika Kusini kundi lote tuliokuwemo kwenye msafara huo tulistaajabu ingawa ilikuwa ni usiku.
Mpangilio wa miji, barabara na huduma ulikuwa ni wa kipekee na wa kisasa jambo kulinganisha na nyumbani au nchi nyingine zote tulizopita.