Prime
Sababu 5 za mtego wa dabi

Muktasari:
- Ukiwasikiliza Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wanasema mchezo huo upo palepale kwamba utapigwa Juni 15 tarehe mpya ambayo ilishatangazwa.
BADO kuna utata juu ya hatma ya mchezo wa kiporo namba 184 kati ya Yanga na Simba ambapo kujua upande mmoja haujanyoosha maelezo kama mchezo upo au haupo hatua ambayo inaweka rehani mechi hiyo.
Ukiwasikiliza Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wanasema mchezo huo upo palepale kwamba utapigwa Juni 15 tarehe mpya ambayo ilishatangazwa. Simba wao wanaendelea na maandalizi wakiwaita watani wao uwanjani lakini Yanga ni kama imeweka ngumu ikionyesha msimamo wake.
Ndani ya Yanga kupitia uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti kuna viashiria vya wazi kwamba dabi hiyo huenda isichezwe;

KAMATI YA UTENDAJI/IDARA YA MASHINDANO
Hili ni eneo muhimu zaidi inapofika kwenye mechi ya watani wa jadi. Kamati ndio kama injini. Mwanaspoti linafahamu kwamba hakuna mpango wowote wa mchezo huo kupitia maelezo ya wajumbe wa juu wa uongozi huo, kwani kikawaida kwenye nyakati kama hizi mambo mengi yalipaswa kuwa yamekamilika.
"Kawaida kwenye mchezo kama huu kuna vikao ambavyo vinakuwa vinafanyika kujipanga na mchezo huo,lakini mpaka sasa hakuna kitu kipya wala mazungumzo ya mechi hiyo na sio kawaida, hakuna mechi hapa fanyeni mambo mengine,"alidokeza bosi huyo wa kamati ya utendaji huku mwingine akiongeza.
"Mimi binafsi huwa kuna majukumu napewa juu ya hiyo mechi lakini mpaka sasa hakuna nililoambiwa na msimamo nadhani unabaki uleule mechi haitapigwa,"aliongeza.
Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kwamba kikawaida kwa zaidi ya wiki tatu kuelekea dabi hata kamati ya mashindano ya klabu huwa bize na hata kwa kuratibu na matawini lakini hilo halifanyiki.
MPANGO KAZI WA KOCHA
Uchunguzi mwingine wa kiufundi,umebaini benchi la ufundi la Yanga nalo lina ratiba ya mechi tatu pekee za mashindano ambapo katika mechi hizo mchezo dhidi ya Simba limejulishwa kwamba haupo.
Bosi mmoja ambaye yupo idara ya ufundi ameliambia Mwanaspoti kwa sharti la kutotajwa gazetini akisema kwenye mechi hizo, wamejulishwa wajiandae na mechi mbili za ligi kati ya Prisons, Dodoma Jiji lakini pia na Fainali ya Kombe la Shirikisho.
"Tumerudi kwenye maandalizi lakini mchezo dhidi ya Simba haupo kwenye ratiba yetu, tulishaambiwa hautakuwepo, tuna ratiba na mechi ya ugenini dhidi ya Prisons na Dodoma na nyingine ya tatu ni ile fainali dhidi ya Singida.
"Unajua kwenye mechi kubwa kama ile (dhidi ya Simba) lazima tujulishwe kwa kuwa ina maandalizi yake maalum kiufundi ni mechi kubwa ambayo sasa maandalizi hayo hayapo kwenye ratiba yetu,"aliongeza.

VIKAO VYA WADAU/MAPATO
Mchezo mkubwa wa Yanga na Simba, kuna vikao vya wadau wakiwemo wa timu hizo mbili, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi na Serikali ambapo mpaka unaposoma hapa viongozi wa timu wenyeji hawajashiriki. Kikawaida timu mwenyeji ndiye anayechukua mapato yote na ndiye anayewajibika kuipromoti mechi husika,lakini katika hili Yanga hawajafanya chochote mpaka sasa na hakuna dalili.
RATIBA FUNGA MSIMU
Kama haitoshi, Yanga juzi usiku imetoa kalenda ya mechi zake zilizosalia za mwezi Juni ambazo zinakwenda kuhitimisha msimu ambapo kwenye mechi hizo tatu, hakuna mchezo huo namba 184 dhidi ya Simba.
Ratiba hiyo inaonyesha Yanga itacheza mechi yake ugenini dhidi ya Prisons Juni 18 ambapo baada ya hapo itarudi nyumbani kumalizana na Dodoma Jiji kisha itasubiri fainali ambayo bado tarehe yake haijapangwa.

MATAWINI KUPO KIMYA
Itakumbukwa kuahirishwa kwa mchezo huo wa Machi 8,2025 ni kufuatia tukio la Simba kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo na makomandoo wa timu mwenyeji Yanga.
Hatahivyo,katika maandalizi ya mchezo huo Mwanaspoti limejiridhisha kwamba kwa upande wa viongozi wa matawi ambao ndio hujipanga na maandalizi ya uwanja na kuweka ulinzi kwenye uwanja huo hakuna mpango wowote kuhusu mechi hiyo ya Juni 15.
"Mnauliza nini kaka, hakuna mechi hapa kama unavyoona kila mtu anaendelea na majukumu yake binafsi wakati kama huu tungekuwa tayari wengine wako Avic (Kambi ya Yanga, Kigamboni) na wengine tungekuwa uwanjani lakini hata mkienda uwanjani hamtakuta mtu," alisema kiongozi huyo wa matawi ya Yanga.

TAMKO LA YANGA
Akizungumza na Crown FM, kuhusu hatma ya mchezo huo na mawasiliano yao na bodi ya ligi Meneja wa Habari wa Yanga Ally Kamwe alisema:"Sisi tuna mawasiliano na bodi ya ligi na kuelekea dabi sisi tumeshatoa msimamo wetu na tumeshaweka ratiba zetu za kumaliza msimu huu."
"Huu Mjadala umeshafungwa na itakuwa vibaya sisi kurudiarudia kitu kilekile,sisi hatuihofii Simba, wala timu yoyote ile kwa sababu sisi ndio tunaongoza ligi na tunaweza kuifunga timu yoyote."
NINI KITATOKEA?
Kufuatia Yanga kushikilia msimamo wa kutocheza mechi hiyo ya dabi, inaweza kuwa nafasi kubwa kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Yanga inabanwa na Kanuni ya 31 ya Ligi Kuu Bara Toleo la 2024 kifungu cha 1 (1.3) inayoelezea adhabu kwa timu itakayoshindwa kufika uwanjani itapokwa pointi 15.
Lakini mgomo huo wa Yanga kuna hatari kwao kupoteza nafasi ya pili itakayowapa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao endapo itateleza katika mechi zilizobaki kisha Azam ikafanya vizuri.

KANUNI HII HAPA
Kanuni ya 31 ya Ligi Kuu Bara Toleo la 2024, kipengele (1) kinasema: “Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF/TPLB na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo: 1.1 Kutozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000/-) ambapo shilingi milioni mbili na laki tano (2,500,000/-) itachukuliwa na Bodi ya Ligi Kuu na shilingi milioni mbili laki tano (2,500,000/-) italipwa kwa timu pinzani.
“1.2 Kulipa fidia ya maandalizi/uharibifu wowote unaoweza kujitokeza. 1.3 Kupokwa alama 15 (kumi na tano) katika msimamo wa Ligi na viongozi waliosababisha jambo hilo watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu. 1.3.1 Endapo timu itakuwa na alama pungufu ya 15, itakuwa na alama hasi kwa kiasi kinachopungua kwenye msimamo wa Ligi.
“1.3.2 Endapo timu itamaliza msimu wa Ligi ikiwa na alama hasi, itaanza na alama hizo hasi katika msimamo wa Ligi kwenye msimu unaofuata wa Ligi ya hadhi yake. 1.4 Itapoteza haki ya kuchukua gawio lake la mapato ya mchezo huo.
“1.5 Kiongozi yeyote atakayebainika kushiriki, alishawishi au alikuwa chanzo au sababu ya timu kutotokea uwanjani bila ya sababu za msingi atafungiwa kwa kipindi cha miezi kumi na miwili (12).
“1.6 Inaweza kukabiliwa na adhabu zaidi kama ambavyo TFF/TPLB itahitaji kuchukua hatua zaidi kadiri itavyoona inafaa. 1.7 Timu yoyote iliyopewa adhabu ya faini chini ya kanuni 31:1(1.1, 1.2 na 1.3) haitaruhusiwa kucheza hadi itakapotekeleza adhabu hiyo kwa daraja ambalo itakuwa ipo.”