Rostand yametimia
Muktasari:
- Walishapiga kelele kuhusu kipa huyo kisha mabosi na makocha wao wakataka kumtoa kwa mkopo African Lyon aliyowahi kuichezea kabla ya kutua Jangwani, haikuwezekana na sasa kipigo cha 3-2 toka kwa Gor Mahia kimempa tiketi Mcameroon huyo kutemwa rasmi.
MASHABIKI wa Yanga wanajua kabisa kikosi chao msimu huu kiko vibaya, lakini wanaamini kipa Youthe Rostand anakabiliwa na changamoto zaidi.
Walishapiga kelele kuhusu kipa huyo kisha mabosi na makocha wao wakataka kumtoa kwa mkopo African Lyon aliyowahi kuichezea kabla ya kutua Jangwani, haikuwezekana na sasa kipigo cha 3-2 toka kwa Gor Mahia kimempa tiketi Mcameroon huyo kutemwa rasmi.
Yanga imetumia saa mbili tu kufanya maamuzi magumu ya kusitisha rasmi mkataba wa kipa huyo namba moja wa kikosi chao, akitimuliwa sambamba na kocha wake, Juma Pondamali na fasta mabosi wakashusha makocha wawili wapya kikosini.
Mabosi wa Yanga juzi Jumapili wakati mchezo wa timu yao dhidi ya Gor Mahia walijikuta katika wakati mgumu wakipokea lawama kubwa kutoka kwa mashabiki wao juu ya uwezo mdogo wa Rostand.
Baada ya mchezo huo kumbe kikao flani cha vigogo kikafanyika na kuamua kumsitishia mkataba kipa huyo, ambaye katika mechi nne za Kombe la Shirikisho hatua ya makundi amejikuta akiruhusu jumla ya mabao 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema kwa sasa klabu yao imeshindwa kumvumilia Rostand baada ya hatua ya kutolewa kwa mkopo kukwama.
Yanga ilitaka kumtoa kwa mkopo Rostand kumrudisha Lyon kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili lakini hatua hiyo ilikwama kutokana na pande hizo mbili kushindwa kukubaliana katika mshahara ya kipa huyo.
Kilichokwamisha ni kwamba Rostand anapokea kiasi cha Dola 1200 (sh 2.7 milioni) kwa mwezi, lakini Lyon ikashindwa kukubaliana na kiasi hicho ambapo uwezo wao ulikuwa ni kumlipa kiasi kisichozidi Dola 300 (sh 700,000) hatua ambayo ilikwamisha uhamisho huo.
Nyika alisema katika mchezo wa juzi walikuwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, George Mkuchika, ambaye naye alishindwa kukubali uwezo wa Rostand.
Bosi huyo alisema jana kulikuwa na kikao baina ya kipa huyo na Mtendaji Mkuu Omary Kaya kuhakikisha wanapitia upya mkataba wa Rostand na kwamba hawataweza kuendelea naye.
Alisema maamuzi hayo hayajatokana na Yanga kupoteza mchezo wa juzi na kwamba tayari uongozi wao uliliona hilo na kuanza kusajili kipa mpya Mkongomani Nkizi Kindoki Klaus.
“Uongozi umechukizwa na kiwango cha Rostand, sio jambo zuri kumtaja mtu timu inapopoteza lakini mechi ya jana imethibitisha kwamba hatukukosea kuleta kipa mpya mapema, pia maamuzi yetu ya kutaka kumtoa yalikuwa sahihi,” alisema.
“Tunakutana naye leo (jana) nafikiri hatutakuwa naye kwa msimu ujao tunatambua kwamba kwa sasa kuingiza mbadala wake katika michuano ya Kombe la Shirikisho itakuwa ngumu lakini ni bora tubaki na makipa wawili tulionao ukiondoa Rostand ambao bado ni makipa wazuri.”
MAKOCHA WAPYA
Katika kuiboresha timu hiyo Nyika alisema kabla ya ligi kuanza kamati yao imelazimika kuvunja benki kuhakikisha inashusha makocha wawili, mmoja mzawa na mwigine wa kigeni ili kumsaidia Mwinyi Zahera na kuimarisha benchi la ufundi.
Nyika alisema wanataka kumshusha Kocha Msaidizi namba moja wa Zahera ambaye lazima awe mzawa ili kuchukua nafasi ya Shadrack Nsajigwa ambaye mkataba wake ulimalizika.
Awali Yanga ilimpokea Kocha Mkongo Gay Bukasa ambaye aliondoka kimyakimya hata kabla hawajamalizana naye.
Muda mrefu Mwanaspoti linafahamu kwamba Yanga ilikuwa katika mpango wa kumpa ajira kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime kuja kusaidiana na Zahera akiambatana na Mzambia Noel Mwandila.
Mbali na kocha huyo pia Nyika alisema wanataka kumalizana haraka na kocha Mkenya wa makipa Razack Siwa ambaye alitua nchini wiki iliyopita anayekuja kuchukua nafasi ya Juma Pondamali.
“Tunataka kuongeza nguvu katika benchi letu, tunataka pia kuongeza kocha mmoja mzawa atakayeungana na Mwandila kumsaidia kocha Zahera lakini pia tunaona kuna mashaka ya kiufundi katika kocha wa makipa.
“Kama mlivyoona kwasasa tupo katika mazungumzo ya mwisho na kocha Siwa nafikiri sasa tutamalizana naye ili aje aanze kazi haraka kupandisha viwango vya makipa wetu,” alisema.