Rekodi ya Simba Queens inatisha WPL
Muktasari:
- Katika mechi hizo 27, mabingwa hao wameonyesha ubora katika safu zote, wakifunga mabao 65 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 15 pekee, huku wakiendelea kuonyesha uimara unaowafanya kuwa miongoni mwa timu zinazotazamwa zaidi katika mbio za ubingwa msimu huu.
SIMBA Queens inaendelea kutengeneza rekodi ya kipekee katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), baada ya kufikisha mechi 27 mfululizo bila kupoteza, ikishinda 23 na sare nne, rekodi inayoifanya kuwa timu pekee iliyocheza mechi nyingi bila kupoteza tangu msimu uliopita.
Katika mechi hizo 27, mabingwa hao wameonyesha ubora katika safu zote, wakifunga mabao 65 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 15 pekee, huku wakiendelea kuonyesha uimara unaowafanya kuwa miongoni mwa timu zinazotazamwa zaidi katika mbio za ubingwa msimu huu.
Mara ya mwisho Simba Queens kupoteza mechi ilikuwa Machi 18, 2025, walipokutana na Yanga Princess kwenye Uwanja wa KMC Complex na kukubali kipigo cha bao 1-0, lililofungwa dakika ya 48 na mshambuliaji Jeanine Mukandayisenga.
Tangu kipigo hicho, kikosi hicho hakijapoteza tena mechi ya ligi, jambo linaloonyesha mwendelezo wa kiwango bora na ushindani unaoendelea kuonyeshwa na wachezaji wake.
Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo, Kocha mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' amesema lengo lao kubwa msimu huu ni kuhakikisha wanatetea ubingwa walioutwaa na wanaendelea kupambana ili kufanikisha dhamira hiyo.
Amesema wanatambua safari ya kutetea taji hilo haitakuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa uliopo msimu huu na ubora wa timu pamoja na usajili uliofanywa na wapinzani umeongeza ugumu wa ligi.
"Malengo yetu ni kutetea ubingwa, tunafahamu ligi imekuwa ngumu kutokana na ubora wa timu na usajili uliofanywa na timu mbalimbali. Hilo linatufanya tuendelee kupambana kuhakikisha mambo yanakuwa sawa na tunafikia malengo yetu," amesema Mgosi.