Prisons, KMC katika mtihani mpya Championship
Muktasari:
- KMC iliyowahi kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019-2020, ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita 2025-2026 na kwa sasa imeonekana kuwa mwiba mkali ikiwa kileleni mwa msimamo.
HADI sasa ni KMC pekee ambayo haijapoteza mechi katika tisa za Ligi ya Championship msimu huu 2026-2027, huku Tanzania Prisons ikiahidi kuisimamisha zitakapokutana Jumapili hii.
KMC iliyowahi kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019-2020, ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita 2025-2026 na kwa sasa imeonekana kuwa mwiba mkali ikiwa kileleni mwa msimamo.
Katika raundi tisa zilizochezwa, timu hiyo ya Halamashauri ya Kinondoni, Dar es Salaam, imeshinda tano na sare nne, ikivuna pointi 19 na wikiendi hii itakuwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kuikabili Prisons.
Prisons ambayo ilishuka daraja msimu uliopita, katika mechi tisa imepoteza mbili sawa na sare, huku ikishinda nne na kuwa nafasi ya tatu kwenye msimamo ikikusanya pointi 17.
Kiungo mshambuliaji wa Prisons, Lambert Sabiyanka, alisema pamoja na ugumu wa mechi hiyo kutokana na mwenendo wa wapinzani, hawatafanya makosa kuhakikisha KMC nayo inachapika.
Alisema kinachowapa nguvu na matumaini ni kutokana na matokeo waliyonayo na kwa sasa ni mapema kutamba kurejea Ligi Kuu msimu ujao licha ya hesabu na ndoto zao ni kufanya hivyo.
“Ni mechi ngumu lakini yenye umuhimu sana haswa kwetu, tunajua KMC hawajapoteza mchezo na sisi tunataka pointi tatu kujiweka pazuri, hatutarajii kufanya makosa yoyote kuhakikisha tunafikia malengo.
“Tumejipanga kama ambavyo tunafanya wakati mwingine na ndoto zetu ni kuona tunarudi Ligi Kuu, haitakuwa mechi nyepesi ila tunazitaka pointi tatu kwakuwa mzunguko wa kwanza ni wa hesabu,” alisema kiungo huyo.
Aliwaomba wadau na mashabiki wa timu hiyo jijini Mbeya kuendelea kuwasapoti, akibainisha kuwa ligi bado haijaisha na hesabu haijatimia, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake aone namna ya kuweka nguvu.