Pazi: Simba ikiamua lake hakuna wakuizuia
'KWA Simba hii hakuna wa kuizuia kufanya jambo lake', hiyo ni kauli ya kocha wa makipa wa zamani wa timu hiyo, Idd Pazi kwamba kupata ushindi sio ishu na nijambo ambalo mashabiki wao wamelizoea.
Simba imetwaa taji la Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo na huu wa nne ina asilimia kubwa kwani ndio inayoongoza kileleni licha ya kuwa nyuma michezo kadha dhidi ya Yanga, inayokutana nayo Julai 3, mwaka 2021.
Pazi ameliambia Mwanaspoti, leo Jumanne ya Juni 29, mwaka 2021 kwamba Simba kuifunga Yanga sio ishu labda itokea Wanajangwani wakapata ushindi ndio itakuwa habari ya mjini kwani ndio wana hamu ya kuonja raha zinazoendelea Msimbazi.
"Mwelekeo wa ubingwa upo Simba kutokana na kubakiza michezo mingi, inaongoza kwa pointi na mabao, jambo linalowafanya mashabiki na wapenzi wa soka kujiamini,hiyo mechi ya Julai 3, Simba haina wasiwasi kutokana na kuwa na kikosi kizuri na chaushindi ndani ya dakika 90 kwa hiyo kushinda kwao sio stori mpya ndio maana nimesema labda itokeee Yanga ikashinda ndio itashangaza,"amesema na ameongeza kuwa;
"Yanga inapaswa kukisuka kikosi chake vyema kwa ajili ya msimu ujao ili kuwafanya mashabiki wao watembee kwa amani na inapocheza wawe na uhakika wa kupata matokeo kama Simba ambayo inajiamini kutokana na ubora wa kikosi chake,"amesema.
Amesema japokuwa mechi ya watani wa jadi haitabiriki, ila anaiona Simba itakuwa inajiamini zaidi kutokana na mwenendo wake na imecheza na timu mbalimbali zenye uwezo mkubwa.
"Nikisema timu zenye uwezo mkubwa nazungumzia na jinsi ambavyo ilikuwa inafanya vyema hata mbele ya timu ngumu michuano ya Caf," amesema.