Oryx Gas kuongeza zawadi, bingwa Main FM Cup kunyakua Sh3 milioni
Muktasari:
- Mbali na fedha hizo, mshindi wa kwanza atazawadiwa jezi, kikombe na medali, huku wachezaji wa timu mbili zitakazofika fainali wakinufaika pia na mitungi ya gesi kutoka kwa mdhamini huyo.
Kampuni ya Oryx Gas imeongeza hamasa katika mashindano ya Main FM Cup yanayoendelea mkoani Kigoma kwa kutangaza zawadi mbalimbali kwa timu zitakazomaliza katika nafasi tatu za juu, huku bingwa akijipatia Sh3 milioni.
Mbali na fedha hizo, mshindi wa kwanza atazawadiwa jezi, kikombe na medali, huku wachezaji wa timu mbili zitakazofika fainali wakinufaika pia na mitungi ya gesi kutoka kwa mdhamini huyo.
Mkuu wa Idara ya Mauzo na Masoko wa Oryx Gas, Shaaban Fundi, alisema kampuni hiyo imeamua kuongeza zawadi hizo ili kuhamasisha ushindani na kuunga mkono maendeleo ya soka katika jamii.
Akizungumza wakati wa kutangaza zawadi hizo katika Uwanja wa Mwanga Kawawa, Ujiji, Kigoma, Fundi alisema mshindi wa pili atapata Sh1.5 milioni, jezi na medali, huku timu itakayomaliza nafasi ya tatu ikizawadiwa Sh1 milioni pamoja na jezi.
Alisema zawadi hizo ni sehemu ya udhamini wa kampuni hiyo ambao pia unalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kupitia gesi ya LPG.
“Tumeamua kutumia jukwaa la soka si tu kuburudisha, bali pia kuwapelekea wananchi wa Kigoma kampeni kabambe ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia,” alisema Fundi.
Alifafanua kuwa katika msimu huu, Oryx Gas imeweka kambi maalumu uwanjani ambako zaidi ya mitungi 500 ya gesi inatarajiwa kugawiwa kwa mashabiki na wananchi.
Alisema wataalamu wa kampuni hiyo wamekuwa wakitumia mapumziko ya mechi na muda kabla ya michezo kutoa elimu ya vitendo kuhusu matumizi ya gesi, usalama wake na faida za kuachana na mkaa na kuni.
Kwa mujibu wa Fundi, mpango huo unalenga kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na yenye gharama nafuu.
Aliongeza kuwa wanajivunia kushirikiana na Main FM katika kuandaa mashindano hayo ambayo, mbali na kutoa burudani, yanasaidia kuibua vipaji vipya vya soka na kuimarisha mshikamano wa jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Main FM, Pascal William, aliipongeza Oryx Gas kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo kwa mwaka wa pili mfululizo, akisema ushirikiano huo umechangia kuongeza hamasa na kufanikisha malengo ya mashindano.
William alisema mashindano hayo yamefikia hatua ya robo fainali baada ya kushirikisha jumla ya timu 16, huku mchezo wa fainali ukitarajiwa kufanyika Novemba 28.
“Tunajisikia fahari kushirikiana na Oryx Gas katika kufanikisha mashindano haya. Mwitikio ni mkubwa na malengo yetu ya kuinua vipaji na kutoa elimu kwa jamii yanatimia,” alisema William.