Omary Kapilima aibukia Bigman FC
Muktasari:
- Katika mechi tatu za Bigman FC ilizocheza, imepoteza zote, ikianza kuchapwa na IAA SC mabao 2-1, ikachapwa 3-1, dhidi ya KMC FC, kisha ikapoteza tena 2-1, mbele ya maafande wa Transit Camp na kushika nafasi ya 15, kwenye msimamo bila pointi.
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa KenGold, Omary Kapilima anakaribia kujiunga na Bigman FC iliyoweka kambi jijini, Tanga kwa ajili ya msimu huu wa 2026-2027 wa Ligi ya Championship, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Amanzi Nurdin.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapilima amesema bado hajafikia makubaliano rasmi ya kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo ambayo zamani ilijulikana kwa jina la Mwadui FC, japo mazungumzo ya awali yameshafanyika na yamebakia mambo machache tu.
"Ni kweli tuko katika mazungumzo hayo kwa ajili ya kuifundisha ila sijasaini mkataba wowote, nimewasili Tanga na muda wowote kuanzia sasa tunaweza tukakamilisha baadhi ya taratibu, ikiwemo suala nzima la masilahi yangu," amesema Kapilima.
Amanzi alijiunga na Bigman FC akitokea Bandari Tanzania, aliyoipandisha Championship msimu wa 2026-2027, huku akiichezea Majimaji FC, Njombe Mji na Ruvu Shooting, wakati nje ya nchi amecheza Karonga United ya Malawi na Aigle Noir ya Burundi.
kwa upande wa Kapilima aliyewahi kufundisha na kucheza timu mbalimbali zikiwemo za Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar, ni miongoni mwa makocha wenye uwezo mkubwa, huku akibeba matumaini ya kikosi hicho kinachosaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu.
Katika mechi tatu za Bigman FC ilizocheza, imepoteza zote, ikianza kuchapwa na IAA SC mabao 2-1, ikachapwa 3-1, dhidi ya KMC FC, kisha ikapoteza tena 2-1, mbele ya maafande wa Transit Camp na kushika nafasi ya 15, kwenye msimamo bila pointi.