Nyota kadhaa Simba wabaki Dar, sababu yatajwa
Muktasari:
- Wachezaji saba wa Simba ambao wako kwenye majukumu ya timu za taifa uwezekano wa kuwahi kambi hiyo haupo, hivyo hawataenda Afrika Kusini na badala yake wataungana na wenzao wakirejea Dar es Salaam.
SIMBA imeanza safari ya kwenda Afrika Kusini kwenye kambi yao fupi ya siku 10 kujiandaa na mechi za mashindano tofauti zijazo, lakini hasa mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga utakaochezwa Oktoba 10, 2026, hata hivyo msafara wao una makundi matatu, huku nyota saba wakizuiwa Dar es Salaam na hawataungana na wenzao huko.
Kwenye msafara wa kwanza uliondoka nchini jana asubuhi, kulikuwa na wachezaji nane ambapo wote wakiwa wazawa wakiongozwa na kocha msaidizi, Seleman Matola.
Kundi hilo liliwahusisha kipa Hussein Abel, mabeki Abdulrazak Hamza, David Kameta ‘Duchu’, Wilson Nangu, Nickson Kibabage wakiwemo pia viungo Semfuko Charles, Kelvin Nashon na mshambuliaji Ismail Mgunda.
Wachezaji hao nane wanakwenda kuungana na mastaa wawili wa kigeni raia wa Afrika Kusini, kiungo Neo Maema na beki Rushine De Reuck ambao wao tayari wapo huko walipokwenda tangu walipopewa mapumziko.
Msafara wa pili kutoka hapa nchini utaondoka leo Ijumaa asubuhi na mwingine wa tatu kesho Jumamosi ambao utawahusisha wachezaji wa kigeni ambao walishaanza kurudi nchini jana alfajiri wakitoka kwenye mapumziko mafupi.
Wachezaji hao sababu ya kuchelewa kuondoka pamoja na wenzao ni kutokana na utaratibu wao wa kuingia Afrika Kusini kutahitaji visa ambazo zilianza kushughulikiwa jana kwa wale ambao walirejea siku hiyo alfajiri.
Simba itaweka kambi ya siku 10 Jiji la Polokwane nchini Afrika Kusini ambapo ndani ya muda huo itapambana kutafuta mechi zisizopungua mbili za kirafiki ambazo zitakuwa ni maalum kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji wa timu hiyo.
SABA WAZUIWA
Wachezaji saba wa Simba ambao wako kwenye majukumu ya timu za taifa uwezekano wa kuwahi kambi hiyo haupo, hivyo hawataenda Afrika Kusini na badala yake wataungana na wenzao wakirejea Dar es Salaam.
Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally, ameliambia Mwanaspoti kuwa, wachezaji hao ambao wengi wanaweza kuwa wamemaliza majukumu ya timu za taifa Septemba 30, 2026, haitakuwa rahisi kwao kuwahi kambi.
Ahmed amesema kambi ya Afrika Kusini itafungwa Oktoba 4, 2026, ambapo watarejea haraka nchini ili kuwapa wachezaji nafasi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa wakitoka jijini Polokwane.
“Wachezaji ambao wako kwenye majukumu ya timu za taifa wao hatutaweza kuungana na timu Afrika Kusini, wakimaliza majukumu yao watarudi moja kwa moja hapa nchini, wataungana na wenzao wakiwa hapa,” amesema Ahmed.
“Tumefanya hivi kutokana na ufinyu wa muda kutoka wakati ambao watakuwa wamemaliza mechi za timu za taifa na hapa tunazungumzia zile mechi zitakazoishia Septemba 29, kama kuna nchi itacheza mechi za kirafiki hapo muda utaongezeka zaidi.”
Wachezaji wa Simba walipo timu ya taifa ya Tanzania ni beki Nathaniel Chilambo, viungo Morrice Abraham na Yusuf Kagoma huku wengine watatu wakiwa timu za vijana chini ya miaka 20 na 23 ambao ni Antony Mligo, Vedastus Masinde, Bakari Msimu na Bashiri Kibaila.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni ambao wako timu za taifa ni kipa Mahamadou Kassali wa Niger na kiungo Inno Loemba anayeitumikia Congo Brazzaville.