Ndejembi atamani ushindani wa Yanga, Simba kuhamia kwenye Kikapu
Muktasari:
- Ndejembi amesema amekubali ombi la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda la kuwa mlezi wa timu za Mpira wa Kikapu alilomuomba wakati anatoa hotuba yake alipoalikwa akiwa mgeni rasmi.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi amesema anatamani kuona siku moja ushindani wa timu za Yanga, Simba, Azam FC na nyingine ukihamia kwenye Mpira wa Kikapu nchini kwa lengo la kuukuza.
Ndejembi ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Oktoba 18, 2026, wakati akiwa mgeni rasmi katika Fainali ya Mpira wa Kikapu inayohusisha Dar City na Stein Warriors.
"Lengo langu siku moja nikuona Mpira wa Kikapu unapiga hatua kubwa kama Mpira wa Miguu ulivyo kwa Yanga na Simba. Hii itawezekana ikiwa wadhamini watajitokeza kuwekeza na vijana wataonyesha utayari wao," amesema Ndejembi.
Aidha, Ndejembi amesema amekubali ombi la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda la kuwa mlezi wa timu za Mpira wa Kikapu alilomuomba wakati anatoa hotuba yake alipoalikwa akiwa mgeni rasmi.
"Nimekubali ombi la kuwa mlezi kwa sababu naupenda Mpira wa Kikapu. Lengo ni kuona unapiga hatua kubwa kama ilivyo michezo mingine nchini inavyozidi kustawi," amesema Ndejembi.
Awali akitoa hotuba yake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema mpira wa Kikapu umepiga hatua kubwa na moja ya malengo yake makubwa ni kuona kunakuwa na viwanja vikubwa vitatu (Arena), vitakavyotoa nafasi ya kuandaa mashindano mbalimbali.
Katika fainali hiyo inayochezwa kwenye Uwanja wa International School Of Tanganyika (IST), Masaki, jijini, Dar es Salaam, mgeni rasmi ni Makamu wa Rais, Deogratius John Ndejembi, aliyeambatana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Maji, Juma Aweso, Waziri wa Kilimo, Daniel Godfrey Chongolo na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabeet.