Namungo, Mashujaa kazi ipo
LIGI Kuu Bara inaendelea tena leo zikipigwa mechi mbili za raundi ya nne, wakati jioni Geita Gold itaialika KMC kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita, huku Namungo ikijitafuta mbele ya Mashujaa Kigoma ambayo inacheza kwa msimu wa kwanza ligi hiyo na huku inaonekana kuwa ya moto!
Geita na KMC zitaumana saa 10:00 jioni, huku ile la Namungo na Mashujaa itapigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Majaliwa, uliopo Ruangwa, mkoani Lindi.
Kwenye mchezo wa Nyankumbu wenyeji, Geita wanavaana na KMC iliyotoka kupoteza mechi iliyopita mbele ya Kagera Sugar, huku KMC ikishinda mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, hivyo mchezo wa leo utakuwa ni vita kwa timu hizo katika msako wa pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Hii itakuwa ni mechi ya tano kwa timu hizo kukutana, kwani katika mechi nne za awali Geita imeshinda mbili na kupoteza moja, huku mchezo mwingine ukiisha kwa sare na kocha wa Geita, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ana kazi ya kuvuna pointi tatu kwenye uwanja wa nyumbani kwani mechi tatu zilizopita walicheza ugenini, wakati KMC huu ni mchezo wa tatu kucheza ugenini.
Ukiachana na mchezo huo, kwenye Uwanja wa Majaliwa, Namungo itakuwa ikisaka pointi tatu za kwanza ikiwa nyumbani, kwani ilipoteza mechi kwa JKT kisha kutoka sare na KMC kabla ya kufungwa ugenini na Yanga kwa bao 1-0.
Kocha Cedrid Kaze atakuwa na kibarua kigumu za kuikabili Mashujaa inayonolewa na Mohammed Abdallah ‘Baresi’ kwani timu hiyo katika mechi tatu zilizopita za awali imeshinda mbili na kutoka sare moja ikiwa ni moja ya timu nne ambazo hazijapoteza ikiungana na vigogo, Yanga, Simba na Azam FC.
Mashujaa imepanda ligi msimu huu kutoka Ligi ya Championship sambamba na JKTTZ na Tabora United.