Namungo kufanya mapinduzi benchi la ufundi
Muktasari:
- Mandla ni miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kujiunga na Namungo FC kwa ajili ya kurithi mikoba ya Juma Mgunda ambaye mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026 mkataba wake unafikia ukomo huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza tena.
UONGOZI wa Namungo FC ‘Wauaji wa Kusini’, umeanza mchakato wa kutafuta kocha mpya kwa ajili ya msimu ujao, huku miongoni mwa majina yanayopewa nafasi ni la Mandla Qhogi, raia wa Afrika Kusini anayekinoa kikosi cha Nsingizini Hotspurs FC ya Eswatini.
Mandla ni miongoni mwa makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kujiunga na Namungo FC kwa ajili ya kurithi mikoba ya Juma Mgunda ambaye mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026 mkataba wake unafikia ukomo huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza tena.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Namungo zimeliambia Mwanaspoti mazungumzo hayo na kocha Mandla yapo, ila hayajafikia hatua za mwisho kwa sababu hadi sasa timu hiyo haina uhakika wa kubaki katika Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2026-2027.
“Ni kweli mazungumzo hayo yapo, lakini kama unavyojua tunachopambana nacho kwa sasa ni kuhakikisha tunabaki kwanza Ligi Kuu na ndipo mambo mengine yafuate. Nadhani mwisho wa msimu huu tutakuwa na majibu sahihi juu ya hilo,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman amesema ni mapema kuzungumzia mustakabali wa benchi lao la ufundi au wachezaji wanaomaliza mikataba kwa sababu msimu bado haujaisha na wanapambana na janga la kushuka daraja.
Licha ya kauli ya Ally Suleiman, Mwanaspoti linafahamu kuwa uongozi wa Namungo FC hauridhishwi na kiwango kinachoendelea kuonyeshwa na Kocha Mgunda ambaye hadi sasa hajapata ushindi wowote katika Ligi Kuu Bara tangu Januari 31, 2026.
Timu hiyo imecheza mechi 15 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga KMC FC bao 1-0 Januari 31, 2026. Kati ya mechi hizo, imepoteza nane na kutoka sare saba, huku ikiwa nafasi ya 13 na pointi 25.
Kiujumla, timu hiyo msimu huu wa 2025-2026 imecheza jumla ya mechi 25 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo imeshinda tano tu, ikitoka sare 10 na kupoteza 10, ikishika nafasi ya 13 na pointi 25 huku ikifunga mabao 19 na kuruhusu 28.
Mgunda aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali ikiwemo Coastal Union na Simba, alijiunga na Namungo FC Oktoba 25, 2024 na mkataba wake unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026 huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.
Kwa upande wa Mandla anayetajwa kuchukua nafasi ya Mgunda, ni kocha kutoka Afrika Kusini anayeheshimika baada ya kuiongoza Nsingizini Hotspurs FC kufikia mafanikio ya kihistoria ya kutwaa mataji matatu (treble) msimu wa 2025-2026.
Katika msimu wake wa kwanza na klabu hiyo, Mandla alishinda Kombe la 8Bet Trade Fair, Kombe la Ingwenyama na Ligi Kuu ya MTN (MTN Premier League), ikiwa ni mafanikio makubwa katika karia yake tangu ajiunge na kikosi hicho Juni 1, 2025.
Mandla alitumia miaka 17 akiwa mkufunzi muhimu wa maendeleo ya wachezaji na kocha wa timu ya DDC (DStv Diski Challenge) katika Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, akisifika kwa kugundua vipaji vya Lyle Foster na Relebohile Mofokeng.
Pia, Mandla aliwahi kuhudumu kama kocha wa Milford FC inayoshiriki ligi za madaraja ya chini Afrika Kusini, huku akipenda kutumia mfumo wa kiufundi wa 4-3-3.