Mwalusako: Ngassa poa tu
Muktasari:
- Mwalusako aliyeichezea Yanga kwa mafanikio miaka ya 1980, alisema bado kiwango cha Ngassa kipo juu na ndio maana mabosi wa klabu hiyo wamemrejesha kwa vile vijana waliopewa nafasi wameshindwa kufanya la maana.
WAKATI baadhi ya mashabiki wa soka wakiishangaa Yanga kuamua kumrejesha kikosini nyota wake wa zamani, Mrisho Ngassa, kutoka Ndanda FC, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wana Jangwani, Lawrance Mwalusako, amebariki ujio wa winga huyo mwenye mbio.
Mwalusako aliyeichezea Yanga kwa mafanikio miaka ya 1980, alisema bado kiwango cha Ngassa kipo juu na ndio maana mabosi wa klabu hiyo wamemrejesha kwa vile vijana waliopewa nafasi wameshindwa kufanya la maana.
“Sioni tatizo kwa Ngassa kurejeshwa kikosini, tangu alipoondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Msuva, hakuna mchezaji mwingine aliyemudu kuvaa viatu vyake, hivyo kwangu ni sahihi kurudi nyumbani,” alisema Mwalusako.
“Unaposajiliwa Yanga au Simba, lazima mchezaji ujitambue na kujitathimini kuwa nyuma yako unafuatiliwa na mamia ya watu, lakini baadhi ya wachezaji waliopo sasa ni kama hawajui thamani ya jezi za timu hizo, Ngassa atawafundisha.”
Mwalusako pia amemtaka Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, kutumia taaluma yake kuwaweka sawa vijana klabuni hapo.