Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mubiru, Sillah wafungua akaunti ya mabao Azam

AZAM Pict

Muktasari:

  • Ushindi huo umepatikana katika mchezo wa mzunguko wa sita wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

BAADA ya kutoa asisti mbili dhidi ya Kagera Sugar, nyota wa Azam FC, Hassan Mubiru leo Septemba 7, 2026 amefungua akaunti yake ya mabao Ligi Kuu Bara sambamba na Gibril Sillah katika ushindi wa 2-0 mbele ya Namungo FC.

Ushindi huo umepatikana katika mchezo wa mzunguko wa sita wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Ni ushindi uliowapa mwendelezo mzuri Azam nyumbani kwani imeshinda mechi zote tatu msimu huu ikizifunga TRA United (2-1), Pamba Jiji (2-1) na Namungo (2-0).

Mubiru na Sillah ambao wote wamejiunga na Azam msimu huu, mabao hayo yamekuwa ni kama kukaribishwa ndani ya Ligi Kuu Bara, licha ya Sillah kuwahi kucheza na kuondoka, huku mwenzake ikiwa ni mara ya kwanza. Kumbuka mechi iliyopita Azam iliposhinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar ugenini, Mubiru alitoa asisti mbili kwa mabao ya Zidane Sereri na Feisal Salum 'Fei Toto'.

AZA 01

Kuanzia filimbi ya kwanza, Azam ilionekana ikiwa na kiu kubwa ya kufunga mabao mengi. Wachezaji wa timu hiyo walifanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Namungo, lakini ukuta wa mabeki pamoja na kiwango cha kipa Suleiman Abraham viliwafanya wapate wakato mgumu.

Hatimaye dakika ya 28 Azam ikafanikiwa mpango wake. Kiungo Kipre Junior alipokea mpira katikati ya uwanja, akasogea kwa kasi na kufika kwenye eneo la hatari. Alipiga shuti kali lililookolewa na Abraham, lakini mpira ulimrudia Hassan Mubiru ambaye kwa utulivu aliutumbukiza golini. Ni bao la kwanza kwa Azam leo na la kwanza kwa Mubiru msimu huu.

Namungo nayo ilijaribu kujibu lakini ulinzi wa Azam ukiongozwa na mabeki wake, nahodha Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Nathan Fasika na Twalibu Nuru ulisimama kidete. Kipa Zuber Foba aliendelea kuonyesha kiwango cha juu kwa kuokoa hatari chache zilizojitokeza, hivyo kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili mchezo ulikuwa mkali zaidi. Feisal Salum ‘Fei Toto’ alipata nafasi nzuri baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Gibril Sillah, lakini alishindwa kuidhibiti vyema na mpira ukaishia mikononi mwa kipa Abraham.

Sillah naye alikuwa na nafasi yake ya dhahabu dakika za mwisho za kipindi cha pili. Alipata pasi kutoka kwa Enock Molia ndani ya boksi, lakini kabla hajapiga beki Hance Masoud aliingilia kwa wakati na kuutoa mpira nje, ikawa kona.

Kipre Junior alijaribu kuongeza bao kwa Azam baada ya kupokea mpira kutoka kwa Molia na kupiga shuti kali, lakini Abraham alionyesha uhodari kwa kunyoosha mikono na kuutoa mpira. Kipa huyo wa Namungo alikuwa miongoni mwa wachezaji bora uwanjani licha ya timu hiyo kupoteza.

AZA 02

Dakika ya 90+5, ndipo Azam ilifunga bao la pili. Donovan Makoma alianza mpira na kumpatia Molia, naye alimuachia Gibril Sillah, aligeuka kwa haraka na kufunga bao la pili, likiwa ni bao la kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ushindi huo umeifanya Azam kupanda hadi pointi 14 baada ya mechi sita, na inasalia nafasi ya tatu kwenye msimamo. Ipo nyuma ya Yanga na Simba ambazo zina pointi 15 kila moja, lakini zimecheza mechi tano.

Namungo imesalia nafasi ya 11 ikiwa na pointi sita nayo ikicheza mechi sita, imepoteza nne zikiwemo tatu mfululizo na kushinda mbili, imefunga mabao sita na kuruhusu 10.

Kipa Zuber Foba ameendelea kung’ara kutokana na leo kutoruhusu bao katika ushindi huo wa 2-0 dhidi ya Namungo. Hii ni clean sheet yake ya pili katika mechi tatu alizocheza. Awali alikuwa langoni kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Geita Gold na ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.