Msigwa, Zitto, Heche wamlilia Hans Poppe
Msemaji Mkuu wa Serikali na wanasiasa maarufu nchini wamemlilia aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Zakaria Hans Poppe aliyefariki dunia jana usiku.
Kupitia mtandao wa Twitter na Instagram wameandika salamu zao za rambirambi na kuelezea namna walivyomfahamu kiongozi huyo mkubwa wa soka nchini.
Msigwa ameandika; "Nimeshtushwa sana na kifo cha Ndugu Zacharia Hans Poppe. Tumepoteza mdau muhimu kwa soka la nchi yetu na mtu aliyetamani kuona Tanzania inakaa kwenye viwango vya kimataifa vya soka,"
"Poleni sana wanafamilia, uongozi wa Simba wachezaji, wapenziwa soka na wanachama wa wapenzi na wote walioguswa na msiba huu,"
Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Vijijini na shabiki wa Simba, John Heche ameandika; "Tanzania imepoteza mtu, Simba imepoteza mtu. Poleni sana familia, nimeguswa sana na msiba wa Mzee Hans Poppe. Mtu ambaye alifikiria vizuri kuhusu nchi yetu, alipenda demokrasia, mara ya mwisho nilimuendesha kwenye gari tukienda kuangalia mechi ya Simba na Gwambina RIP kamanda,"
Zitto Kabwe ameandika pumzika kwa amani Zakaria Hans Poppe.
Godbless Lema aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini ameandika; "Hans Poppe alikuwa mtu aliyejiamini na alichukizwa sana na uonevu,"
Aliyekuwa Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa ameandika; "Mpenda mabadiliko, open minded, a good friend of mine ! Rest in peace mnyaluko. Watu wa Iringa tumepoteza moja ya shujaa wetu. We will miss you,"
Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA yeye ameandika; "Pigo kubwa kwa jamii ya wapenda michezo, hasa mpira wa miguu, ukapumzike kwa amani Mzee Zakaria Hans Poppe. Niwaombee moyo wa ustahamilivu familia yake na wapenda michezo nchini. Tumuombee. Mungu amempenda zaidi,"