Moto wa Iddi Nado Azam FC
KAMA kuna mchezaji anayeendelea kuthibitisha ubora wake ndani ya kikosi cha Azam FC hivi sasa, basi ni winga Iddi Selemani ‘Nado’.
Nyota huyo amekuwa na kiwango bora tangu msimu ulipoanza, akifanya uamuzi kwenye mechi ngumu na kugeuka kuwa silaha muhimu kwa matajiri wa Chamazi.
Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Nado ameonekana kuwa na mchango muhimu kwa Azam FC. Katika mchezo wa kwanza dhidi ya ZED FC nchini Misri, alionyesha ukomavu wake kwa kuifungia Azam bao la ugenini kupitia shuti kali na kuilazimisha timu hiyo kutoka sare ya 1-1, matokeo yaliyoiweka katika nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano.
Timu hiyo iliporejea Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Nado alifanya kilekile kwa kupiga shuti jingine la hatari lililotikisa nyavu za wapinzani na kuipa Azam ushindi wa bao 1-0. Matokeo hayo yaliwafanya watinge hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo, kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Mabao yote mawili aliyofunga Nado kwenye michezo hiyo ya mchujo wa kimataifa hayakuwa tu ya ushindi, bali yalikuwa na umuhimu mkubwa katika safari ya Azam FC. Pia, yote yalitokana na mashuti ya umbali mrefu.
Nado anaendelea kuonyesha ubora wake hadi kwenye Ligi Kuu, ambako mpaka sasa ameshafunga mabao matatu, akionyesha mwendelezo mzuri wa kiwango chake tangu kuanza kwa msimu huu.
Ubora wa Nado upo katika namna anavyoweza kusoma mchezo na kutumia nafasi anazopata nje ya eneo la hatari. Uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali umekuwa silaha kubwa inayowapa wakati mgumu walinzi wa timu pinzani.
Msimu uliopita, katika mechi 23 alizocheza za ligi, alifunga mabao nane na kutoa asisti nne, akihusika katika mabao 12 ya timu yake.
Akizungumza kuhusu kiwango chake, Nado amesema: “Namshukuru Mungu. Kimsingi, fomu yangu kwa sasa naamini si mbaya na si nzuri zaidi, kwa hiyo bado tunapambana kuhakikisha inakuwa vizuri zaidi. Malengo yangu si mengi, ni kuifanya timu yangu iweze kufanikiwa kufunga mabao ambayo imejiwekea. Ila lengo langu ni kuhakikisha natoa mchango mkubwa katika timu yangu na kufanikisha malengo hayo ya kufunga mabao,” amesema Nado na kuongeza:
“Kwenye maono yangu, tunaweza kusonga zaidi ya hatua tuliyoishia awali. Kwa hiyo naamini tunaweza kufika hata robo fainali au, Mungu akitujalia, tunaweza kucheza hata fainali. Namuomba Mungu tuendelee hivi hivi.”
“Kwangu mimi naamini tunaweza kufanya kitu kwenye msimu huu kwa sababu aliyekuwa juu yetu siamini kama ametuacha kwa pointi nyingi, na mechi bado ni nyingi. Naamini tunaweza kufika na pia kuchukua ubingwa. Siyo jambo gumu.”