Moloko anaitaka namba yake Yanga
WINGA wa Yanga, Jesus Moloko amerejea kwenye kikosi hicho ikiwemo kufanya mazoezi na wenzake na amesema wakati akiwa nje ya uwanja kuna kitu amejifunza na kuyasikia ambayo yamemjenga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Moloko alisema wakati huo alikuwa anasikia kama kuna kitu hakijakamilika kwake haswa wakati akiona Yanga inacheza mechi bila ya uwepo wake ila maisha ya soka ndio yalivyo.
“Wakati nipo nje nafasi ninayotumika kuna wenzangu wamefanya vizuri kuipigania timu ndio maana imefanikiwa kuendeleza rekodi ya kutokupoteza hadi sasa,” alisema Moloko na kuongeza;
“Baada ya kuliona hilo nilianza kufanya mazoezi yangu mengi binafsi ili kurudisha utimamu wa mwili kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kuumia na nashukuru nimeweza kwa kiasi kikubwa.
“Mazoezi hayo binafsi niliyofanya yameongeza kitu hata nilipojiunga na wenzangu baada ya kutoka majeruhi sikuwa katika kiwango cha chini kwani niliweza kufanya mazoezi na programu nyingine bila shida.”
Katika hatua nyingine Moloko alisema alikuwa anafanya hivyo ili kuendelea kuaminiwa na kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa wakati hajapata majeraha hayo ya mguu.
Moloko alisema yupo Yanga kwa ajili ya kuipambania iweze kufanya vizuri kwenye mashindano yote hatamani kuona yupo fiti na anashindwa kupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.
“Ligi bado ngumu imekuwa na ushindani mkubwa zaidi huu mzunguko wa pili ila wachezaji wa Yanga malengo yetu yapo pale pale kupambana kila mechi iliyokuwa mbele yetu na kuhakikisha tunashinda,” alisema Moloko mwenye mabao matatu kwenye ligi na kuongeza;
“Nipo na hamu ya kucheza mechi kutokana ni muda mrefu tangu wakati naumia ila bahati nzuri narejea tukiwa na mechi ngumu dhidi ya Azam kama nikipata nafasi ya kucheza nitapambana vya kutosha.”
Akiwa nje nafasi anayotumika Moloko alicheza, Farid Mussa anayecheza pia kama beki, Chico Ushindi, Dickson Ambundo Denis Nkane na Saido Ntibazonkiza.