Mohamed Laizer aichorea ramani Gunners FC
Muktasari:
- Laizer amejiunga na Gunners FC baada ya kukaa kwa muda bila kufundisha timu yoyote, tangu mara ya mwisho alipoachana na Fountain Gate inayocheza Ligi Kuu Bara, Aprili 10, 2026, akichukua nafasi ya Henry Mkanwa aliyeifundisha msimu wa 2025-2026.
BAADA ya kufikia uamuzi wa kuifundisha Gunners FC ya jijini, Dodoma, kocha mkuu wa timu hiyo, Mohamed Ismail 'Laizer' amesema ni wakati sahihi kwake wa kutengeneza kikosi bora, licha ya ushindani mkubwa uliopo katika Ligi ya Championship.
Laizer amejiunga na Gunners FC baada ya kukaa kwa muda bila kufundisha timu yoyote, tangu mara ya mwisho alipoachana na Fountain Gate inayocheza Ligi Kuu Bara, Aprili 10, 2026, akichukua nafasi ya Henry Mkanwa aliyeifundisha msimu wa 2025-2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema ni jambo nzuri kwake baada ya kufikia makubaliano ya kukifundisha kikosi hicho chenye makazi yake jijini, Dodoma, japo ni changamoto nyingine ya kuhakikisha anafanya vizuri na kutimiza malengo yao.
"Malengo ya timu ni kuipandisha Ligi Kuu Bara msimu wa 2027-2028 na hilo ndio jambo kubwa tunalopigania, siyo rahisi kwa sababu ya ushindani wa Ligi ya Championship, ila kutokana na sapoti ninayoipata tunaweza kutimiza hilo," amesema Laizer.
Laizer aliiongoza Fountain Gate katika mechi 15, za Ligi Kuu msimu wa 2025-2026 na kati ya hizo alishinda nne, sare nne na kupoteza saba, huku timu hiyo ikifunga mabao nane na kuruhusu 18, akiiacha ikishika nafasi ya 14 na pointi zake 16.
Gunners FC inashiriki Ligi ya Championship kwa msimu wa pili sasa tangu ilipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza msimu wa 2025-2026 na kumaliza ikiwa nafasi ya nane na pointi 38, baada ya kushinda mechi 11, ikitoka sare tano na kupoteza 14.