Mnoga vitani kusaka tiketi ya League One England
Muktasari:
- Mechi hiyo itaamua timu itakayopanda kucheza Ligi Daraja la Pili England, EFL League One msimu ujao.
BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Haji Mnoga leo atakuwa na kibarua kizito England wakati chama lake Salford City itakaposhuka dimbani kucheza fainali ya playoff ya ligi daraja la nne 'League Two' dhidi ya Notts County, kwenye Uwanja wa Wembley saa 11 jioni.
Mechi hiyo itaamua timu itakayopanda kucheza Ligi Daraja la Pili England, EFL League One msimu ujao.
Salford City ilitinga fainali baada ya kuitoa Grimsby Town katika hatua ya nusu fainali. Katika mechi ya kwanza, ilishinda mabao 2-1 ugenini kabla ya kutoka sare ya 2-2 na mechi zote hizo Mtanzania huyo alimaliza dakika zote 90.
Licha ya kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa League Two, Salford ilikosa nafasi ya kupanda moja kwa moja kutokana na mfumo wa ligi hiyo unaozipa timu tatu za juu nafasi ya moja kwa moja huku nafasi ya nne hadi saba zikilazimika kucheza playoff.
Kwa upande wa Mnoga, mechi hiyo ni nafasi nyingine ya kuendelea kuandika historia katika soka la England baada ya kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Salford City msimu huu.
Beki huyo anayemudu kucheza nafasi ya beki wa kulia, beki wa kati pamoja na winga wa kulia, ameonyesha kiwango kizuri kilichomfanya kuendelea kuaminiwa kikosi cha kwanza.
Msimu huu, Mnoga amecheza mechi 26 za mashindano mbalimbali kwa dakika 1,787 huku akianza kikosi cha kwanza mara 21 na takwimu zinaonyesha namna alivyokuwa sehemu muhimu ya timu hiyo.
Salford City, inayomilikiwa na mmoja wa nyota wa zamani wa Manchester United, David Beckham, imekuwa na ndoto kubwa ya kupanda daraja.
Iwapo Salford City itashinda leo, Mnoga ataingia kwenye kitabu cha rekodi ya kuwa mmoja ya Watanzania wachache waliowahi kusaidia timu za kupanda madaraja katika mfumo wa soka la England.