Mkakati wa mashujaa breki ya FIFA
Muktasari:
- Kocha Josiah alijiunga na Mashujaa Julai 23, 2026 kuiongoza timu hiyo msimu huu wa 2026-2027 na alipokea kijiti kutoka kwa kocha Jamhuri Kihwelo.
MASHUJAA FC imegeuza breki ya FIFA kuwa fursa ya kurekebisha upungufu uliojitokeza kwenye mechi za mwanzo za msimu, huku kocha Amani Josiah akipanga kuimarisha safu ya ulinzi na kuongeza makali kwenye ushambuliaji.
Kocha Josiah alijiunga na Mashujaa Julai 23, 2026 kuiongoza timu hiyo msimu huu wa 2026-2027 na alipokea kijiti kutoka kwa kocha Jamhuri Kihwelo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah alisema wiki hizi tatu za mapumziko ya ligi, zitampa muda wa kutosha kuwaingiza wachezaji kwenye falsafa yake kwa undani, jambo ambalo hakupata nafasi ya kulifanya vizuri kabla ya msimu kuanza.
“Wiki hizi tatu za breki ya FIFA ni wakati muafaka kwangu kuingiza falsafa zangu kwa undani zaidi, muda ambao haukupatikana kabla kwani pre-season haikutupa nafasi kubwa ya kujinoa,” alisema Josiah.
Kocha huyo alisema kipaumbele chake ni kuimarisha ulinzi kwa kupunguza makosa na kuongeza umakini wa wachezaji, hasa katika namna ya kuzuia wapinzani wanapofika kwenye maeneo hatari.
Mbali na ulinzi, Josiah alisema anataka pia kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji ili timu iwe na ufanisi zaidi katika kutumia nafasi na kubadilisha fursa kuwa mabao.
“Katika jukumu hilo tunataka kuimarisha safu yetu ya ulinzi, pia kuipa makali safu yetu ya ushambuliaji, ili tuweze kufunga na kuzuia mashambulizi ya wapinzani.” alisema.
Mashujaa imecheza mechi sita za Ligi Kuu Bara msimu huu 2026-2027, ikishinda michezo mitatu dhidi ya Coastal Union (1-0), Kagera Sugar (2-1) na Singida Black Stars (2-1), huku ikipoteza mitatu dhidi ya Fountain Gate (1-0), Mbeya City (2-1) na Dodoma Jiji (1-0).
Sasa kazi iliyopo ni kuhakikisha maboresho hayo yanaonekana uwanjani baada ya breki ya FIFA, huku Mashujaa ikitarajiwa kurejea na kukutana na Polisi Tanzania Oktoba 8, 2026 ambapo ligi itarejea.