Mchezaji amtumia meseji nzito Ngoma
Muktasari:
- Chambua alisema uwezo wa Ngoma kwa sasa hautishi kama msimu uliopita
MWANACHAMA na mchezaji wa zamani anayeheshimika ndani ya Yanga, Sekilojo Chambua ameutazama uelekeo wa straika wa Yanga, Donald Ngoma kisha akamtolea ya moyoni ambayo akiyasikia yatamsaidia kubadilika uwanjani.
Chambua alisema uwezo wa Ngoma kwa sasa hautishi kama msimu uliopita, alipotua klabuni hapo na kumtaka asijisahau na kujifananisha na wazawa, kwani yeye ni mchezaji wa kigeni na ana heshima yake na anakoelekea mashabiki watamchoka.
“Achilia mbali kusumbuliwa na majeraha, ukweli ni kuwa Ngoma anatakiwa kujituma ili asichokwe na mashabiki, ajue yeye ni mchezaji wa kigeni na thamani yake iko wapi, akitaka kuwa kama wazawa nadhani uelekeo wake hautakuwa sahihi, atapotea” alisema.
Awali, alisema Ngoma alikuwa anategemewa na klabu na wapinzani walikuwa wanaogopa uwepo wake uwanjani, lakini kwa sasa acheze asicheze wanamchukulia kawaida jambo alilosema ni dalili mbaya kwa staa kama yeye.
“Ndiyo maana asilimia kubwa kwa sasa anakumbukwa Amissi Tambwe kutokana na rekodi aliyoiweka msimu uliopita, mchezaji mwingine ambaye hajasahaulika kwa mashabiki ni Simon Msuva, hilo liwe funzo kwake,” alisema.
Ngoma amepachika mabao mawili msimu huu tofauti na uliopita ambao, alionekana kuwa machachari zaidi na kuwa gumzo kila kona ya nchi ilipokuwa ikikanyaga Yanga.
Benchi la ufundi limekuwa likimlinda kwa maelezo kwamba, majeruhi yalimtoa kwenye fomu huku wakisisitiza ni jambo la kawaida kwenye soka na wanaamini kuwa atarudi muda si mrefu kwenye kutupia kwa kasi.