Mashujaa Queens kuiheshimu Simba, lakini yalenga ndoo
Muktasari:
- Matokeo hayo yameongeza matumaini ndani ya kikosi hicho, lakini sasa kinahitaji kuthibitisha uwezo wake wa kuendeleza kasi hiyo kitakapokabiliana na Simba Queens, ambayo imekuwa miongoni mwa timu zinazoongoza soka la wanawake nchini.
NAHODHA wa Mashujaa Queens, Sabina Emmanuel amesema licha ya timu yake kuanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), wanatambua ubora wa Simba Queens na hawataichukulia kirahisi watakapokutana Novemba 11 kwenye Uwanja wa NDC, Mbweni.
Sabina amesema wanauheshimu uwezo na uzoefu wa Simba katika ligi hiyo, hivyo wamejipanga kwa umakini kukabiliana na mpinzani huyo huku wakiahidi kutoa ushindani ili kupata matokeo mazuri.
Amesema lengo la Mashujaa msimu huu ni kutwaa ubingwa, jambo linalowalazimisha kupambana na timu kubwa kama Simba, kwani michezo ya aina hiyo ndiyo inayoweza kupima uwezo wao wa kugombea taji.
“Lengo la mwaka huu ni ubingwa, hivyo kama tunataka ndoo lazima tushindane na vigogo kama Simba. Tunaendelea na maandalizi na tunajua utakuwa mchezo mgumu, lakini tutaenda kupambana,” amesema Sabina.
Mashujaa Queens inaingia katika mchezo huo ikiwa na mwanzo mzuri baada ya kuanza kampeni zake kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fountain Gate Princess, kabla ya kuichapa Kilimanjaro Wanderers mabao 2-1.
Matokeo hayo yameongeza matumaini ndani ya kikosi hicho, lakini sasa kinahitaji kuthibitisha uwezo wake wa kuendeleza kasi hiyo kitakapokabiliana na Simba Queens, ambayo imekuwa miongoni mwa timu zinazoongoza soka la wanawake nchini.