Mashabiki Yanga, Simba wakamiana
Muktasari:
- Mashabiki Yanga, Simba wa Mwanza wafunga safari kuishudia mechi kesho
Mwanza. Homa ya pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga limepamba moto kwa mashabiki wa vigogo hao nchini kwa kila upande kutamba timu yao kuibuka na ushindi.
Wapinzani hao wanatarajia kuvaamna kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo kila timu itaingia kwa kumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wao wa mwisho.
Wakizungumzia mpambano huo mashabiki wa pande zote jijini Mwanza, walitamba kuwa lazima waibuke na ushindi kutokana na ubora wa vikosi vyao.
Mashabiki wa Yanga tawi la Mwanza Mjini kupitia kwa Katibu wake, Mhando Madega alisema kuwa imani yao ni ushindi na tayari wamesafiri kwenda Dar es Salaam kuisapoti timu yao.
Alisema kuwa jumla ya mashabiki 45 wameifuata timu yao kwa malengo ya kuishangilia mwanzo mwisho ili kuwazima wapinzani.
“Tayari mashabiki 45 kutoka Mwanza tumesafiri tangu jana Alhamisi kwenda kuisapoti timu yetu matumaini yetu ni kuhakikisha Simba hawaambulii chochote,” alisema Madega.
Mwenyekiti wa Simba tawi la Mwanza, Omary Makoye alisema kuwa licha ya mchezo huo kuonekana kuwa mgumu, lakini lazima Simba iibuke na ushindi.
“Mchezo unaonekana kuwa na ushindani, lakini kwa ubora wa Simba ya msimu huu, Yanga wajiandae kisaikolijia na tayari mashabiki 37 tumeenda kuishangilia timu yetu,” alisema Makoye.