Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapema tu Mwarabu anakaa!

LICHA ya kwamba ni mechi ya kusaka heshima, Simba imesisitiza kuwa inataka kuwapa raha mashabiki wake kwa kuupiga mwingi na kupata ushindi ugenini mapema tu dhidi ya Al Ahly, jijini Cairo.

Simba itakaribishwa na Al Ahly katika mchezo wa kukamilisha ratiba kundi A utakaopigwa kuanzia saa 2:00 usiku Al-Salam WE uwanja unaomilikiwa na wenyeji badala ya ule wa Kimataifa wa Cairo uliozoeleka, huku takwimu ilizoweka mechi tano zilizopita zikiibeba kutaka kuandika rekodi ya kupata ushindi mara ya kwanza Cairo.

Simba na Mamelodi Sundowns ndizo hazijapoteza mechi katika makundi, kila moja ikishinda nne na kutoka sare moja na kukusanya pointi 13 zikiongoza makundi yao na pia Simba ikiwa na ukuta chuma kwa kuruhusu bao moja tu.

Hata kwenye safu ya ushambuliaji, Simba sio wanyonge kwani wako nafasi ya tatu katika orodha ya timu zilizofunga idadi kubwa ya mabao katika mashindano hayo nyuma ya Al Ahly na Mamelodi ambazo kila moja imepachika 10 huku yenyewe ikiwa imefunga mabao tisa.

Simba inaingia uwanjani ikifahamu ushindi utawapa heshima kubwa ya kumaliza utemi wa muda mrefu ambao Al Ahly wamekuwa nao pindi wanapocheza mechi za kimataifa katika ardhi ya Misri. Al Ahly haijafungwa Cairo tangu walipolala mabao 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas katika mechi ya makundi ya michuano hiyo Juni 28, 2016 na kipindi chote hicho imecheza mechi 31 ikishinda 24 na kutoka sare saba ikifungwa mabao 75 ikiwa ni wastani wa mabao 2.42, huku ikiruhusu nyavu kutikiswa mara 16 tu ikiwa ni wastani wa bao 0.52

Mechi hiyo pia ni ya kisasi, kwani kila timu itakuwa na hamu ya kulipiza kisasi kwa kumbukumbu za michezo ya nyuma.

Al Ahly ina hamu ya kulipa kisasi cha kulala 1-0 ugenini msimu huu, lakini Simba ikiwa na hasira za kufungwa 5-0 walipokutana mara ya mwisho jijini Cairo, Februari 2, 2019.

Katika mchezo huo kama kuna mtu ambaye Simba wanapaswa kuwa makini naye zaidi basi ni refa Mustapha Ghobal kutoka Algeria, kwani ni mwepesi wa kutoa kadi na hata adhabu za penalti pindi wachezaji wafanyapo makosa.

Katika mechi 10 za Ligi ya Mabingwa Afrika alizowahi kuchezesha tangu 2018, ametoa kadi 56 ikiwa ni wastani wa kadi 5.6 katika kila mchezo ambapo kati ya hizo za njano ni 54 na nyekundu ni mbili. Pia katika mechi hizo ametoa penalti saba na rekodi zinaonyesha aliwahi kutoa penalti katika mechi sita mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika kile kinachoonekana ni kupanda kwa homa ya mechi hiyo kwa wenyeji, kuna mabadiliko ya uwanja utakaochezewa ambayo yametangazwa hivi karibuni na Al Ahly.

Tofauti na Uwanja wa Kimataifa wa Cairo ambao Al Ahly wameutumia katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Al Merrikh na AS Vita Club, mechi dhidi ya Simba itachezwa Uwanja wa Al-Salam WE unaomilikiwa na klabu hiyo. “Wachezaji wetu watakusanyika El Tetsh leo (jana) kuanza maandalizi ya mechi hiyo itakayochezwa Ijumaa kuanzia saa 3.00 usiku (saa 4.00 usiku kwa muda wa Tanzania.

“Kikao cha kiufundi cha mechi kitafanyika Alhamisi (jana) saa 8.00 Alasiri katika makao makuu ya Al Ahly yaliyopo Gezira, Cairo,” alithibitisha mkurugenzi wa Mpira wa Miguu wa Al Ahly, Sayed Abdelhafiz, juzi kupitia tovuti na kituo cha luninga cha klabu hiyo.

Simba yenyewe jana ilifanya mazoezi na kocha Gomes ameonyesha kuingiza kikosi chake kikiwa na mabadiliko kadhaa hasa eneo la kiungo na ushambuliaji kwa nia ya kutaka kuwalinda wachezaji wake.

Gomes huenda akawapumzisha wachezaji kadhaa ili kujiandaa na robo fainali inayotarajiwa kupangwa Aprili 30 na kuchezwa kati ya Mei 14-22.

Nyota wanaweza kupumzishwa leo ni Chris Mugalu, Lwanga Taddeo, Clatous Chama na Luis Miquissone ambao nafasi zao zinaweza kuchukuliwa na Meddie Kagere, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga na Francis Kahata. “Tuna mchezo ulio mbele yetu dhidi ya Al Ahly. Ni mchezo ambao tunahitaji kupata matokeo mazuri na malengo yetu ni kutumia kikosi chetu kamili katika mchezo huo na sio kufanya mabadiliko makubwa kwani tunahitaji kushinda,” alisema Gomes aliyesisitiza watapambana kwa soka tamu kama Dar es Salaam na kupata ushindi wa kulinda heshima yao.

“Hata hivyo hilo litategemea na hali za wachezaji kuelekea katika mchezo huo kwani kuna muda wa takribani wiki upo mbele yetu hivyo tutaangalia itakavyokuwa,” alisema Gomes aliyesisitiza licha ya kufuzu robo fainali wanatamani kushinda pia mechi hiyo.

Wakati Simba ikiwa na kikosi kamili, majeraha yanaiandama Al Ahly baada ya mshambuliaji Walter Bwalya kuumia katika mazoezi ya juzi na yupo kwenye hatihati ya kucheza. Pia timu hiyo itawakosa Hamdy Fathy na Ali Maaloul wanaouguza majeraha.