Prime
Manula katikati ya timu nne

Muktasari:
- Hakuna ubishi kuwa ubora wake ulionekana kuanzia akiwa na Azam FC, Simba wakamuona na kumchukua kwenye timu yao kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
AISHI Manula ni moja ya makipa bora zaidi kuwahi kutokea hapa nchini kwa miaka ya hivi karibuni.
Hakuna ubishi kuwa ubora wake ulionekana kuanzia akiwa na Azam FC, Simba wakamuona na kumchukua kwenye timu yao kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
Kiwango chake kwenye klabu pamoja na timu ya Taifa, Taifa Stars ni kielelezo tosha kuwa huyo ni mmoja kati ya makipa bora kuwahi kutokea hapa nchini.
Katika misimu minne nyuma ambayo kipa huyo alikaa langoni kwenye kikosi cha Simba, wastani wake wa kuruhusu mabao kwenye ligi ulikuwa ni chini ya 20, msimu ambao aliruhusu mabao mengi zaidi ni 2023/2024 ambapo alifungwa mabao 25 msimu mzima huku 2022/2023 akiruhusu mabao 17, 2021/2022 akifungwa 14 sawa na 2020/2021.

Kama unataka kuzungumzia kuhusu mafanikio ya Simba kwa kipindi chote chini ya tajiri Mohammed ‘MO’ Dewji basi huwezi kuacha kulitaja jina la Manula kutokana na ubora ambao amefanikiwa kuuonyesha kwenye ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.
Kabla ya kutua Moussa Camara katika kikosi cha Simba mwanzoni mwa msimu huu, misimu zaidi ya sita ambayo Simba ilifanya mapinduzi kwenye soka la Afrika langoni alikuwa akikaa Manula, alikosekana mara chache sana na pengo lake likaonekana.
Hakuna anayefahamu kilichomkuta kipa huyo ambaye alikuwa panga pangua kwenye kikosi cha Taifa Stars kabla hajaondolewa hivi karibuni kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba.
Kwa msimu huu, ameonekana kwenye mchezo mmoja tu wa kirafiki dhidi ya Al Hilal ambao alicheza kwa dakika 45 na kuonyesha kiwango cha juu, baada ya hapo imebaki historia, amekuwa akionekana mazoezi, lakini kwenye kila mechi za Simba amekaa jukwaani kwenye benchi akikaa Ally Salim.

Mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilikuwa muhimu kwa timu hiyo, bado Manula alikaa jukwaani akiwa amevaa kitambulisho shingoni, siyo kipa mdogo ni yule ambaye amefanikiwa kuipitisha Simba kwenye nyakati zote ngumu, lakini uvumilivu wake ukampa medali ya Kombe la Shirikisho bila kucheza, siyo kosa lake.
Juzi alionekana akiwa jukwaani wakati wa fainali ya mashindano ya vijana chini ya miaka 20, kati ya Azam na Fountain Gate na mashabiki wa Azam wakamshangilia huku wengine wakiamini kuwa anastahili kutua kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu.
Taarifa zinaonyesha kuwa baada ya msimu kumalizika, Manula ambaye alisahaulika hata kutajwa jina wakati wa Tamasha la Simba Day ataondoka kwenye kikosi cha Simba kwa kuwa mkataba wake na wekundu hao wa Msimbazi utamalizika, je anaweza kupata nafasi wapi.?
AZAM FC
Hii ni timu ya kwanza ambayo Manula atakuwa na uhakika wa kupata nafasi ya kucheza na kuwa msaada mkubwa kama atatua hapo mwishoni mwa msimu huu.
Tangu ameondoka hakuna kipa ambaye amepatikana mwenye kiwango bora, Ali Ahmada alitua Azam kama mfalme na kuonyesha ubora wa juu mwanzoni lakini mwisho mambo yalikuwa magumu kwake na kuruhusu mabao rahisi baadaye akaondolewa na kupelekwa kwa mkopo KMC.

Baada yake alionekana kuwa Abdulai Idrissa anaweza kuvaa viatu vyake, naye mambo yameonekana kuwa magumu kwake akiwa pamoja na Zubeir Foba, naye ni hivyohivyo hafikii kiwango cha Manula, hivyo kwa kuwa timu hiyo inakwenda kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baadaye mwaka huu ni sahihi kuwa Manula ni chaguo bora kwao kwa kuwa anaweza pia kuisaidia kwenye suala la uzoefu wa michuano ya kimataifa jambo ambalo limekuwa tabu kwa Azam miaka yote.
Kwenye Ligi Kuu, Azam imeshindwa kuwania nafasi mbili za juu kutokana na kuruhusu mabao mengi ikiwa hadi sasa bado mechi mbili msimu umalizike imeshafungwa mabao 17.
SINGIDA BS
Kwa sasa Singida wana kipa bora, Amos Obasogie raia wa Nigeria ukweli akikaa na Manula vita itakuwa kubwa, lakini tetesi zinaonyesha kuwa yupo njiani kujiunga na Yanga endapo tu Djigui Diarra atondoka mwishoni mwa msimu huu.
Hapa ni sehemu nyingine ambayo ni muhimu kwa Manula kwa kuwa pia Singida inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni timu changa zaidi kwenye mashindano hayo, hivyo huyu atakuwa msaada mkubwa kwao.
Kuondoka kwa kipa huyo inamaana kuwa Singida haitakuwa na kipa mwingine mwenye ubora wa juu zaidi ya Manula na hivyo litakuwa chaguo sahihi kwao, kwenye kucheza pamoja na kuendelea kuwasaidia makipa chupukizi wa timu hiyo, lakini pia mbinu za uzoefu wake kwenye michuano ya kimataifa ni jambo lingine muhimu.
YANGA
Hakuna shaka kuwa Diarra ni kipa wa kiwango cha juu, lakini kuna gepu kubwa sana kati yake na makipa wanaofuata kwenye timu hiyo.
Kama Yanga inataka kuwa na makipa bora kwenye kikosi hicho kwa kuwa msimu ujao itakuwa na mashindano mengi, haijalishi kama Diarra ataondoka au atabaki lakini uhalisia ni kwamba Manula anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Diarra na kama ataondoka na Yanga wakaona kuna ugumu wa kumpata Obasogie basi huyo anaweza kuwa kipa namba moja kwenye timu hiyo au namba mbili kutokana na uzoefu, pamoja na ubora alionao, lakini hili litakuwa daraja kwake pia kujiandaa kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho mwezi Agosti kitashiriki michuano ya CHAN.
SIMBA
Hakuna shaka kama siyo mambo ya nje ya kiwango, Aishi Manula bado ana nafasi kubwa ya kuitumikia Simba na kupata nafasi angalau asilimia 50 ya michezo yote kwenye msimu wa ligi.

Simba kwa sasa kipa wake namba moja ni Moussa Camara ambaye kwenye Ligi Kuu tayari ameshaonyesha kiwango cha juu akiwa ameruhusu mabao 11 na kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Lakini kuna gepu kubwa sana kati ya Camara na kipa namba mbili Ally Salim, ambaye kwenye mchezo mmoja dhidi ya Singida wikiendi iliyopita aliruhusu mabao mawili.
Bado Simba wanaweza kumshawishi Manula akabaki klabuni hapo kwa msimu mwingine mmoja akipewa nafasi anaweza kufanya mambo makubwa hata kama Camara atabaki au ataondoka nafasi ya kipa huyo mzawa inaonekana.