Mangungu aibuka na hoja uchaguzi Simba
Muktasari:
- Mangungu ameyasema hayo jana Oktoba 29, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
WAKATI Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, ameibua hoja kuhusu uhalali wa mchakato wa uchaguzi mkuu ndani ya klabu hiyo, Kamati ya uchaguzi imewataka wanachama wenye sifa kwenda kuchukua fomu na kuwasilisha maombi yao kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Mangungu ameyasema hayo jana Oktoba 29, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Mchakato huu ambao umetangazwa ni mchakato batili na haramu,” amesema Mangungu.
Amesema hana nia ya kumuondoa mtu yeyote ndani ya Simba, bali anataka klabu hiyo isonge mbele kwa kufuata taratibu zilizowekwa. Hata hivyo, amedai kuwa baadhi ya watu wanaomshauri mwekezaji wanaweza kuwa wanachangia kukwama kwa mchakato huo, bila kuwataja kwa majina.
“Mimi sijawahi kuwa na nia na sitakuwa na nia hiyo ya kumuondoa mtu yoyote ndani ya Simba. Nataka Simba iweze kwenda mbele na kufuata masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu,” amesema.
AHOJI UKIMYA WA TFF, BMT
Mangungu amesema anashangazwa na namna TFF na BMT zilivyokaa kimya kuhusu suala hilo, akitaka mamlaka hizo kuchukua hatua na kuchunguza uhalali wa mchakato huo kwa kuzingatia taratibu zinazotumika katika masuala ya klabu nyingine.
Amesema Simba ni taasisi kubwa inayotegemewa na watu wengi na yenye nafasi muhimu katika kuunganisha Watanzania, hivyo amewataka wanachama na mashabiki kuepuka kauli zinazoweza kuibua hisia na kusababisha misukosuko.
AWEKA MZANI WA KATIBA
Katika hoja nyingine, Mangungu amewataka wadau wa Simba kusoma katiba ya klabu hiyo kwa ujumla badala ya kuchukua ibara moja na kuacha nyingine, akieleza kuwa kuna vifungu vinavyohusiana na muundo wa bodi, uhalali wa uteuzi wake na mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu.
Ameitaja Ibara ya 11, akisema inazungumzia mwenyekiti kushauriana na bodi kuhusu kuitisha mkutano mkuu, huku akisisitiza kuwa vifungu vya katiba vinapaswa kutafsiriwa kwa kuzingatia uhusiano wake.
AWATAKA WANASIMBA WATULIE
Mangungu amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kuwa watulivu na kuepuka mipango ya maandamano au hatua nyingine zinazoweza kuibua misukosuko, akisema serikali na mamlaka za soka zinaendelea na majukumu yao.
Hata hivyo, madai ya Mangungu kuhusu uhalali wa mchakato huo yanahitaji kuangaliwa pamoja na maelezo ya TFF, BMT na upande wa mwekezaji ili kupata picha kamili ya mvutano unaoendelea ndani ya Simba.
SIMBA YATOA RATIBA
Muda mchache baada ya Mangungu kuzungumza na waandishi wa habari, Simba SC kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, ilitoa taarifa kwa umma iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka "TANGAZO LA NAFASI ZA KUGOMBEA UONGOZI UCHAGUZI MKUU WA SIMBA SPORTS CLUB 2026."
Taarifa hiyo ilianza kwa kusema: "Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, kwa mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 37 ya Katiba ya Simba Sports Club, Toleo la 2018 (lililofanyiwa marekebisho tarehe 30 Novemba, 2025), na kwa mujibu wa Ibara ya 26(12) na Ibara ya 27 ya Katiba hiyo, inawatangazia wanachama wote wenye sifa za kugombea nafasi za uongozi zitakazogombewa katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu utakaofanyika tarehe 03 Januari, 2027."
Katika uchaguzi huo, nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, mjumbe mmoja wa Bodi ya Wakurugenzi mwenye shahada na wajumbe wanne wa Bodi ya Wakurugenzi.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti anatakiwa kuwa na shahada ya kwanza au sifa inayolingana nayo kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Sifa hiyo pia inahitajika kwa mgombea wa nafasi ya mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi mwenye shahada, huku nafasi nne za wajumbe wengine wa bodi zikihitaji angalau mgombea mmoja kuwa mwanamke.
Aidha, wagombea wote wanatakiwa kuwa wanachama wa klabu hiyo na wawe wamelipa ada ya uanachama kikamilifu. Pia wanapaswa kuwa na elimu inayotakiwa kwa nafasi wanazoomba, kuwa na angalau miaka mitatu ya uanachama na kuwa na umri wa miaka 25 au zaidi, lakini chini ya miaka 65.
Sifa nyingine ni kutokuwa wamewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo, kutokuwa mwamuzi wa mpira wa miguu anayefanya kazi wakati huo, pamoja na kutokuwa mwanachama wa chombo cha haki cha klabu au Kamati ya Uchaguzi kwa kipindi husika.
Kamati hiyo imeeleza kuwa fomu zitapatikana katika ofisi za klabu, huku ratiba ikionyesha kuwa uchukuaji wa fomu utafanyika kuanzia leo Ijumaa Oktoba 30, 2026 hadi Novemba 6, 2026.
Uwasilishaji wa fomu hizo utafanyika kuanzia Novemba 7 hadi 11, 2026, kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Januari 3, 2027.
Aidha, Kamati ya Uchaguzi imeweka wazi kuwa uamuzi wake unaweza kukatiwa rufaa kupitia Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, ambayo uamuzi wake ni wa mwisho.
INAVYOSEMA KATIBA KUHUSU UCHAGUZI
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba ya mwaka 2018 ambayo ilifanyiwa mabarekebisho 2025 na kusajiliwa na Februari 2026, imeweka wazi utaratibu wa kuundwa na utendaji wa Kamati ya Uchaguzi, mamlaka ya kuitisha Mkutano Mkuu, uchaguzi wa viongozi pamoja na namna kura zinavyopaswa kupigwa, ikisisitiza kuwa uchaguzi wa viongozi wa klabu hiyo hufanyika kila baada ya miaka minne.
Kwa mujibu wa Ibara ya 37(1), Kamati ya Uchaguzi huteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi, ikiwa na jukumu la kuandaa na kusimamia uchaguzi pamoja na kuishauri Bodi kuhusu kanuni za uchaguzi. Hata hivyo, kamati hiyo inapaswa kufanya kazi chini ya usimamizi na maelekezo ya Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Katika muundo wake, Ibara ya 37(2) inaeleza kuwa Kamati ya Uchaguzi inapaswa kuwa na wajumbe watano, ambao ni Mwenyekiti, Makamu wa Mwenyekiti na wajumbe wengine watatu. Katiba hiyo pia inaweka sharti kuwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo lazima wawe na taaluma ya Sheria.
Aidha, Ibara ya 11(3) na Ibara ya 29(3) zinaweka zuio kwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kuwa wakati huo huo mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi au Chombo cha Haki cha klabu, hatua inayotenganisha majukumu ya uongozi na yale ya usimamizi wa uchaguzi na utoaji wa haki ndani ya taasisi hiyo.
Kuhusu kanuni zinazotumika katika kusimamia uchaguzi, Ibara ya 37(3) inaeleza kuwa kamati hiyo itatekeleza majukumu yake kwa kutumia Kanuni za Uchaguzi za Simba Sports Club. Endapo kanuni hizo hazipo, Kanuni za Uchaguzi za TFF ndizo zitakazotumika kuongoza mchakato huo.
Katiba pia imeweka masharti ya uhalali wa vikao vya Kamati ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa Ibara ya 37(4), maamuzi ya kamati hiyo yatakuwa halali iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria kikao, huku mmoja wao akiwa lazima Mwenyekiti au Makamu wa Mwenyekiti.
Katika suala la rufaa, Ibara ya 37(5) inaeleza kuwa maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi yanaweza kukatiwa rufaa katika Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, ambayo maamuzi yake yatakuwa ya mwisho.
Katika upande wa uendeshaji wa uchaguzi, Katiba ya Simba imeweka Mkutano Mkuu kuwa chombo kinachotumika kufanya uchaguzi wa viongozi wa klabu hiyo.
Ibara ya 21(1) na Ibara ya 23(1) zinaeleza kuwa Mkutano Mkuu utaitishwa na Mwenyekiti kwa kushauriana na Bodi ya Wakurugenzi. Hivyo, utaratibu wa kuitisha mkutano huo unahusisha mashauriano kati ya Mwenyekiti na Bodi ya Wakurugenzi.
Kwa upande mwingine, Ibara ya 18(2) na Ibara ya 20(6) zinaweka wazi kuwa Mkutano Mkuu ndicho chombo chenye mamlaka ya juu ya kuchagua viongozi wa Simba Sports Club kila baada ya miaka minne.
Uchaguzi wa nafasi zilizo wazi pia umetajwa kuwa sehemu ya ajenda rasmi za Mkutano Mkuu wa Kawaida. Hili limeainishwa katika Ibara ya 22(i), inayotaja uchaguzi wa nafasi zozote zilizo wazi miongoni mwa ajenda zinazopaswa kujadiliwa katika mkutano huo.