Mamsera FC bingwa Mkenda Cup ikiibwaga Kawele FC
Muktasari:
- Mamsera FC imeilaza Kawele FC kwa penalti 5-4 na kutwaa ubingwa wa mashindano yaliyoshirikisha timu 118 wilayani Rombo, huku msanii Mboso akiongeza shamrashamra kwa burudani ya muziki.
Timu ya Mamsera FC imetwaa ubingwa wa mashindano ya mpira wa miguu ya Mkenda Cup, msimu wa nne wa mwaka 2026, baada ya kuilaza Kawele FC kwa mikwaju ya penalti 5-4 katika fainali ya mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 118 wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
Mashindano hayo yameandaliwa na mbunge wa jimbo hilo ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha afya zao kupitia michezo na kuwaunganisha wananchi wa wilaya hiyo kwa pamoja.
Msanii wa Muziki wa Bongo Fleva, Mbwana Kilungi maarufu Mbosso, alikuwa miongoni mwa wasanii waliotumbuiza katika mashindano hayo, akiwaburudisha wananchi waliojitokeza kushuhudia fainali ya Mkenda Cup. Burudani hiyo iliongeza shamrashamra katika hafla hiyo, huku mashabiki wakipata fursa ya kufurahia muziki sambamba na kushuhudia ushindani wa timu hizo zilizowania ubingwa wa mashindano hayo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mashindano hayo leo, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, amewapongeza wachezaji walioshiriki katika mashindano hayo, akisema idadi ya timu zilizoshindana inaonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika michezo hiyo.
Amesema mashindano hayo yalianza katika ngazi ya kata, ambapo timu zilishindana kabla ya kupata nafasi ya kucheza hatua zilizofuata hadi kufikia fainali.
“Nawapongeza wachezaji wote kutoka timu 118 zilizoshiriki mashindano haya. Nawashukuru pia Bodi ya Michezo inayoongozwa na ndugu yetu Themy Masae pamoja na wajumbe wake kwa kazi nzuri ya kusimamia mashindano tangu mwanzo,” amesema.
Aliwapongeza pia waamuzi waliosimamia michezo hiyo, akisema mchango wao ulikuwa muhimu katika kuhakikisha mashindano yanafanyika hadi mwisho.
Profesa Mkenda aliwashukuru viongozi wa mkoa na wilaya, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na madiwani, kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mashindano hayo ambayo yameendelea kuwakuza vijana.
Amesema madiwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia timu za kata zao, jambo lililowezesha wilaya hiyo kuwa na uwakilishi mpana katika mashindano hayo.
CHONGOLO AMPONGEZA MKENDA
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ambaye ndiye mgeni rasmi katika fainali hiyo, amempongeza Profesa Mkenda kwa kuanzisha na kuendeleza mashindano hayo, akisema michezo ina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya vijana na kuleta furaha kwa wananchi.
Amesema michezo si burudani pekee, bali pia ni njia mojawapo ya kupunguza msongo wa mawazo na kuwafanya vijana kuwa na afya bora.
“Nimpongeza mbunge wenu, Profesa Mkenda, kwa uamuzi wake wa kuendesha mashindano haya muhimu ya Mkenda Cup. Ni jambo jema kuwa na kiongozi anayetambua umuhimu wa michezo kwa wananchi wake,” amesema.
Chongolo amesema mashindano hayo yanaonyesha upendo wa mbunge huyo kwa wananchi wa Rombo, kwa kuwa yamewapa vijana nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kushiriki shughuli zinazochangia ustawi wao.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo katika kujenga jamii yenye afya, umoja na mshikamano, hivyo akawahimiza viongozi na wananchi kuendelea kuunga mkono shughuli zinazowashirikisha vijana.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mashindano ya Mkenda Cup, Temmy Masae, amesema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza na kuibua vipaji vya soka katika Wilaya ya Rombo na maeneo mengine, huku yakitoa wachezaji maarufu waliokuja kujenga majina yao katika soka la Tanzania.
Amesema baadhi ya wachezaji waliopitia katika mashindano hayo ni pamoja na Selemani Mwalimu na Ramadhan Chobwedo, ambao ni mfano wa mchango wa mashindano hayo katika kukuza vipaji na kutoa fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao.
Masae amesema lengo la kuendelea kuandaa mashindano hayo ni kuendeleza vipaji vya vijana, kuwapa nafasi ya kushiriki mashindano yenye ushindani na kuweka mazingira yatakayowawezesha wachezaji wenye uwezo kufikia ngazi za juu za soka.