Makosa ya ulinzi yaigharimu Azam FFC CAFCC
Muktasari:
- Azam ilianza mechi hiyo kwa kasi ikitaka kutumia faida ya kucheza nyumbani, lakini ilijikuta ikipoteza mwelekeo baada ya wageni kutumia udhaifu wa safu yake ya beki kupata mabao mawili ndani ya dakika 33 za kipindi cha kwanza.
MAKOSA ya safu ya beki, hasa kuacha mianya nyuma wakati wa kushambulia, ndiyo yaliyoigharimu Azam FC baada ya kukaubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Al Ahly Tripoli ya Libya katika mechi ya kundi B wa Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa jana Ijumaa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Azam ilianza mechi hiyo kwa kasi ikitaka kutumia faida ya kucheza nyumbani, lakini ilijikuta ikipoteza mwelekeo baada ya wageni kutumia udhaifu wa safu yake ya beki kupata mabao mawili ndani ya dakika 33 za kipindi cha kwanza.
Tatizo kubwa lilionekana wakati Azam ilipopanda kushambulia na wachezaji wake walikuwa wakiacha nafasi kubwa nyuma zilizowapa Al Ahly Tripoli fursa ya kufanya mashambulizi ya haraka.
Katika bao la kwanza dakika ya tisa, Al Ahly Tripoli ilitumia nafasi iliyoachwa upande wa kulia wa beki ya Azam, eneo alilokuwa akicheza Lusajo Mwaikenda. Hamdou El Houni ndiye aliyepachika bao hilo kwa asisti ya Muaid Ellafi.
Bao hilo lilipaswa kuwa tahadhari kwa Azam kwa namna ilivyokuwa ikiacha nafasi nyuma, lakini dakika ya 33 wageni walipata bao la pili la Ellafi aliyemalizia pasi ya Mostafa Shakshak, akimalizia kwa kichwa, huku beki ya Azam kumzuia na matokeo kuwa 2-0.
Hata hivyo, Azam ilijaribu kurejea mchezoni dakika ya 43 na ilipata bao lililofungwa na Zidane Sereri na kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Hali hiyo ilimlazimu kocha wa Azam, Florent Ibenge, kufanya mabadiliko ya kiufundi akitaka kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji baada ya kuona timu yake ikihitaji mabao ili kurejea mchezoni.
Awali, Ibenge alikuwa akitumia viungo wawili wenye majukumu ya kukaba, Himid Mao na Sadio Kanoute, lakini baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 aliamua kubadili mfumo kwa kubaki na kiungo mmoja mkabaji.
Katika mabadiliko hayo, Himid Mao alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Kipre Junior, hatua iliyolenga kuongeza nguvu ya ushambuliaji kwa kumpa kocha nafasi ya kuwa na wachezaji wengi zaidi wenye majukumu ya kwenda mbele.
Kipindi cha pili, Azam iliendelea kutafuta bao, huku Ibenge akiendelea kufanya mabadiliko. Dakika ya 59, Hassan Mubiru aliingia kuchukua nafasi ya Abdul Suleiman. Tripoli nayo ilimtoa Lamine Camara dakika ya 62, akaingia Blati Toure.
Hata hivyo, Azam ilishindwa kutumia nafasi ya kucheza nyumbani, huku Al Ahly Tripoli ikilinda uongozi wake wa mabao 2-1 hadi mchezo ulipomalizika.